Na, Mwandishi wetu.
Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi hususani wasichana wapende kusoma zaidi masomo ya Sayansi na Hisabati ili watimize ndoto zao.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa jijini Dar es salaam na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga wakati akifungua kongamano la Waalimu wanaofundisha masomo ya Sayansi na Hisabati.
Katika Kongamano hilo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Ualimu-DUCE na kuandaliwa na Mbunge Kupitia wafanyakazi Janejelly Ntate, Naibu Waziri Kipanga, amesema tayari serikali imeshaanza kuweka mazingira rafiki ikiwa ni pamoja na kuajiri zaidi walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati.
Aidha, mipango mingine ya serikali ni kuanzisha ujenzi wa shule 26 katika kila mkoa nchini kwa ajili ya wanafunzi wa kike watakaosoma masomo ya Sayansi.
Mipango mingine ni ujenzi wa mabweni kwa ajili ya watoto wa kike ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mmomonyoko wa maadili ili watimize ndoto zao.
Aidha, Naibu Waziri Kipanga amesisitiza kuwa mpango mwingine wa serikali ni kuwarudisha shuleni wanafunzi wa kike waliopata changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito ili waendelee na masomo yao kama kawaida.
Kwa upande wake, mwandaaji wa kongamano hilo, Mbunge Janejelly, amesema kwa kuwa yeye ni mtoto wa mwalimu, ameandaa kongamano hilo kutoka kwa walimu wa Mkoa wa Dar es salaam ili kuja majawabu ya kwa nini ufaulu katika masomo ya Sayansi na Hisabati unashuka hapa nchini.
Kupitia kongamano hilo amesema anaamini kuwa walimu watajadili na kuja na majibu yatakayoisaidia serikali ni hatua gani ichukue katika kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo wanafunzi wengi kutopenda kusoma masomo hayo ya Sayansi na Hisabati.