Kiongozi
wa Msafara Bi Catherine Musingwilire asifia juhudi zinazofanywa na SSH na
kusifia Tanzania kuwa ni sawa na nyumbani kwake
· DG
Kashimba aahidi kuendeleza ushirikiano na amefurahishwa na kufarijika na ujio
huo
UJUMBE kutoka Serikali na Bunge la Jamhuri ya Uganda umefanya ziara ya mafunzo PSSSF
kwa ajili ya kujifunza namna ya uendeshaji wa huduma za hifadhi ya jamii kwa waajiriwa
wa Serikali, kufuatia maboresho ya kisera ya kuanzisha Mfuko wa Pensheni kwa
Watumishi wa Umma unaoanzisha rasmi utaratibu wa kuchangia kupitia muswada wa
Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma wa mwaka 2023; uliowasilishwa Bungeni
na Serikali ya Uganda mnamo tarehe 14 Machi 2023.
Akiukaribisha
ugeni huo Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF CPA. Hosea Kashimba alisema amefarijika sana
kwa heshima hiyo na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano na ushauri kila mara
itakapohitajika. Aidha mkuu wa msafara
huo Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Utumishi wa Umma Bi. Catherine
Musingwiire ameushukuru uongozi wa PSSSF kwa kuwapatia elimu na uzoefu wa kina
wa namna bora za uendeshaji wa Mfuko kupitia mifumo ya ukusanyaji michango,
uwekaji wa kumbukumbu za wanachama, huduma za kidijitali za wanachama pamoja na
upande wa uwekezaji ili kuhakikisha uendelevu wa Mfuko.
Mada
mbalimbali ziliwasilishwa na watendaji wa Mfuko wakiwemo Mkurugenzi wa
Uendeshaji Mbaruku Magawa, Mkurugenzi wa Hadhari na Majanga Ansgar Mushi, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Vupe Ligate,
Afisa Mkuu wa Huduma za Sheria Valentino Daudi na Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA
Mariam Saleh. Wawasilishaji hawa
walisisitiza umuhimu wa kuweka mazingira wezeshi kuendana na mabadiliko,
ushirikishwaji wa utatu (Serikali, Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri), utayari
wa kisiasa, huduma bora na matumizi ya teknolojia ili kufanikisha maboresho
hayo ya kisera.
Ujumbe
huo ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Utumishi wa Umma Bi. Catherine
Musingwiire uliambatana na Mhe. Apolot Christine (MB) Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Utumishi wa Umma na Serikali za Mitaa; Mhe. Wokorach Peter
(MB); Mhe. Baatom Koryang; Mhe. Nyangweso Denis (MB); Moses Bekabye mshauri wa
Waziri wa Fedha; Byaruhanga Alex Mwanasheria Mwanadamizi wa Serikali; Opoti
Jalmeo karani wa Kamati ya Bunge ya Utumishi wa Umma na Serikali za Mitaa na
Afisa Ubalozi wa Uganda nchini Bi. Connie R. Nuwagaba.
PSSSF
hivi karibuni pia ilipokea ugeni kutoka Serikali ya Kenya, mashirikia ya
Kimataifa ya IMF na World Bank kupitia ziara ambazo zimejikita kwenye kubadilishana
uzoefu wa kitaalam na kujifunza masuala mbalimbali ya hifadhi ya jamii.