Tume ya Madini yaainisha mafanikio makubwa kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini
Dodoma
Wizara ya Madini kupitia Taasisi za Tume ya Madini, Wakala wa Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) leo Mei 26, 2023 imetoa semina kwa wabunge wanawake kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu Sekta ya Madini pamoja na fursa uwekezaji zilizopo katika sekta hiyo.
Semina hiyo iliyofanyika jijini Dodoma na kufunguliwa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa kwa niaba ya Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko imeshirikisha pia viongozi wengine ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Augustine Ollal, Kamishna wa Madini Nchini, Dkt. Abdulrahman Mwanga na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula.
Viongozi wengine walioshiriki katika semina hiyo walikuwa ni pamoja na Kamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma, Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini, wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini.
Awali akizungumza katika ufunguzi wa semina hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amefafanua kuwa utoaji wa semina kwa wabunge ni mwendelezo wa Wizara katika kuhakikisha wadau wengi wa madini wanapata uelewa mpana kuhusu Sekta ya Madini pamoja na fursa zilizopo.
“ Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kukua kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017 wakati wa uanzishwaji wa Wizara ya Madini hadi kufikia asilimia 9.7 mwezi Machi mwaka huu, hivyo wadau wa madini kutoka ndani na nje ya nchi wanaalikwa kushiriki kwenye shughuli za utafiti, uchimbaji na biashara ya madini ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma za ajira, ulinzi na chakula kwenye shughuli za madini,” amesisitiza Naibu Waziri Kiruswa.
Awali akitoa mada kuhusu fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, Meneja wa Biashara ya Madini, George Kaseza amesema kuwa tangu maboresho ya Sheria ya madini na kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na ongezeko la manunuzi na huduma za ndani ya nchi tofauti na awali ambapo kampuni za madini zilikuwa zikiagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.
“Kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini zimepelekea uanzishwaji wa viwanda vikubwa viwili nchini ikiwa ni pamoja na kiwanda cha Max Steel kinachozalisha wire mesh na bolt na kiwanda cha Rock Solution Limited kinachozalisha makasha ya kuhifadhi sampuli za madini ambavyo vinasambaza bidhaa katika migodi mikubwa ya madini, ongezeko la ajira kwenye migodi ya madini kutoka 6,668 mwaka 2018 hadi 14,308 mwaka 2021 na ongezeko la utoaji wa huduma kwenye migodi mikubwa ya madini hali iliyopelekea kuimarika kwa kipato cha wananchi na Serikali kupata kodi mbalimbali,” amesisitiza Kaseza.
Katika hatua nyingine, Kaseza amefafanua kuwa ili kuhakikisha wananchi wengi wanashiriki kikamilifu kwenye Sekta ya Madini, Tume ya Madini imeendelea kutoa elimu kwa wananchi katika mikoa mbalimbali kwa njia ya mikutano, maonesho na vyombo vya habari ambayo imepelekea kuwepo kwa mwitikio mkubwa wa wananchi kushiriki katika shughuli za madini.
Mada zilizotolewa katika semina hiyo, ni pamoja na Jiolojia ya Tanzania na fursa zilizopo, fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini na shughuli za STAMICO katika kuwasaidia wachimbaji wadogo