Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Willbroad Mutafungwa akionyesha baadhi ya vitu walivyowakamata navyo waganga wakienyeji
..
Na Hellen Mtereko, Mwanza.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia waganga wa kienyeji 33 wanaojihusisha na ramri chonganishi sanjari na kufanya shughuli za uganga wa kienyeji bila kufuata taratibu za kisheria.
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Mei 26, 2023 na Kamanda wa Jeshi hilo, SACP Willbroad Mutafungwa wakati alipokuwa akitoa taarifa ya matukio mbalimbali kwa waandishi wa habari.
Amesema Mei 17, 2023 katika kijiji cha Igunguya Wilaya ya Kwimba askari Polisi wakiwa kwenye msako walifanikiwa kuwakamata Lunyilija Ndila (51) mkulima na mkazi wa kijiji hicho,Mashaka John (36) mkazi wa kijiji cha Bungulwa,Ngeneja Kisinza (45) mkazi wa kitongoji cha Kilyaboya
“Hao ni miongoni mwa waganga 33 walikamatwa kwa nyakati tofauti wakiwa wanafanya shughuli za uganga wa jadi kinyume cha sheria na watuhumiwa wamekutwa na vielelezo mbalimbali walivyokuwa wakivitumia kwa shughuli hizo,watuhumiwa wote wamehojiwa na watafikishwa mahakani baada ya upelelezi kukamilika”, amesema Kamanda SACP Mutafungwa.
Katika hatua nyingine Kamanda Mutafungwa ameeleza tukio la mauaji ya Peter Mang’ela (48) mkazi wa Nyakabungo aliyeuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali baada ya kwenda kudai pesa nyumbani kwa Julias Gain.
” Inadaiwa Februari 25, 2023 muda wa saa mbili usiku Peter Mang’ela alifika nyumbani kwa Julias Gaini kwa lengo la kudai pesa yake shilingi 6,500 ambayo ilikuwa ni deni aliyoinywea pombe na baada ya kufika ulizuka ugomvi baina yao na kupelekea marehemu kushambuliwa”, amesema Kamanda SACP Mutafungwa.
Ameeleza kuwa baada ya tukio hilo Jeshi hilo limefanya ufuatiliaji wa tukio hilo na kuwakamata Julius Gaini,Judith John, Roda Julius kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Peter Mang’ela na upelelezi katika tukio hilo unaendeleaje na watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi ukamilika.