Na Mwandishi wetu, Babati
WAKAZI wa Mkoa wa Manyara, wananufaika kwa kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria bila malipo kwa muda wa siku 10 ili kukomesha migogoro mbalimbali waliyonayo.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Pauline Gekul amezindua huduma hiyo mjini Babati iitwayo kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya upatikanaji wa haki kwa jamii.
Gekul amesema jopo la wasaidizi wa kisheria wa Wizara hiyo watatoa huduma hiyo kwa jamii mkoani Manyara bila malipo kwa muda wa siku 10 kwenye wilaya tano.
“Watu wenye migogoro ya ardhi, migogoro ya ndoa, huduma za kisheria na nyinginezo wafike kutatuliwa matatizo yao bila malipo yoyote yale,” amesema Gekul.
Naibu Katibu mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt Khatibu Kazungu amesema jambo hilo ni muhimu mno katika kuwawezesha wananchi kufikia haki zao za kikatiba na kisheria.
Dkt Kazungu amesema kupitia fursa hiyo jamii itafahamishwa juu ya sheria mbalimbali zinazogusa maisha yao ya kila siku ikiwemo sheria ya ardhi, mirathi, ndoa na sheria ya mtoto.
Mkuu wa wilaya ya Mbulu, Komred Kheri James ambaye amemwakilisha Mkuu wa mkoa huo amewataka viongozi wa kuteuliwa na kuchaguliwa kutoa ushirikiano katika kampeni hiyo ili jamii inufaike.
Komred James amesema viongozi hao wapokee kampeni hiyo na kuwapa ushirikiano wahusika ili ifanikiwe kufika katika maeneo yote watakayopitia.
“Wananchi mnapaswa kujitokeza kuchangamkia fursa hii kwani wengi wenu hamna wanasheria wala mawakili hivyo tumieni nafasi hii kikamilifu,” amesema Komred James.
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Manyara, Regina Ndege amesema kampeni hiyo itawasaidia wanawake na watoto kupata haki zao kwani jamii hasa zilizopo vijijini zinakabiliwa na changamoto nyingi za kisheria.
Mjumbe wa kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Khadija Shabani Keisha amewataka wakazi wa Manyara kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo inayotolewa bure na Serikali.
Mkazi wa Magugu wilayani Babati, John Nade amesema mkoa huo ni miongoni mwa maeneo yanye migogoro mingi ya ardhi hivyo kampeni hiyo itawasaidia.