Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewataka wamiliki wa nyumba zinazokodishwa kuhakikisha zinatumika kwa matumizi sahihi ili kupunguza matendo maovu yanayoendelea nchini.
Mhe. Hemed ameyasema hayo wakati akiwasalimia waumini wa Msikiti wa Mameali Saateni mara baada ya kutekeleza Ibada ya Sala ya Ijumaa.
Amesema kuwepo kwa vitendo viovu nchini ikiwemo udhalilishaji, utumiaji wa dawa za kulevya na mapenzi ya Jinsia moja vinavyofanyika katika baadhi ya nyumba zinazokodishwa ndani ya jamii zetu kunapelekea kuongozeka kwa vitendo hivyo. Hivyo, amesisitiza lazima kuwe na ufuatiliaji wa karibu kwa wapangaji na wamiliki wa nyumba hizo ili kuvitokomeza.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wanachukua juhudi kubwa kupinga vitendo viovu ndani ya nchi yetu ambapo amewataka wananchi kuendelea kuwaunga Mkono kwa kufichua wafanyaji wa vitendo hivyo pamoja na kuacha muhali kwa kutoa ushahidi kwa watuhumiwa watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Pamoja na hayo Alhajj Hemed amewataka wananchi kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kujenga miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji na barabara.
Amesema Serikali imeamua kuzifanyia ukarabati Barabara mbali mbali nchini ili kurahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi pamoja na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.
Aidha Mhe. Hemed amewataka maimamu na mashekhe kuongoza Dua ya kumuomba Allah (S.W) aivushe Zanzibar na vitendo viovu.
Akitoa Khutba katika Sala hiyo Sheikh Muhamed Ayoub Muhamed amewataka waumini kujichunga na maovu hasa katika kipindi hiki cha miezi mitukufu ambacho Mtume Muhammad (S.A.W) alikuwa akikitumia kwa kuzidisha Ibada.
Aidha amewataka waumini hao kushikamana na usia wa Mtume Muhammad (S.A.W) na kumuogopa Mwenyezi Mungu kwa kuacha kutenda mambo ya haramu.