Askofu wa Mashariki na Pwani, Dr. Alex G. Malasusa akizundua jiwe la msingi la Mradi wa “Ijangala Mini Hydropower” kwa niaba ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Baba Askofu, Dkt. Fredrick Onael Shoo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo TIB, Bw. Joseph Chilambo akizungumza wakati wa sherehe za uwekaji jiwe la msingi kwenye mradi wa umeme Ijangala ‘Min Hydropower Project’.
Askofu wa Mashariki na Pwani, Dr. Alex G. Malasusa (wapili kushoto) akimsikiliza mmoja wa wataalamu wanaotekeleza mradi wa umeme Ijangala ‘Min Hydropower Project’. Mradi huo unatekelezwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri kupitia katika kampuni yao Nishati Lutheran DKK yenye makazi yake katika kata ya Tandala, kijiji cha Msisiwe Wilayani Makete Mkoani Njombe. Mradi huo umefadhiliwa na mkopo kutoka Benki ya Maendeleo TIB, ruzuku kutoka kwa Wakala wa Nishati Vijini (REA) pamoja na wahisani mbalimbali wa Kanisa hilo.
Na Mwandishi Wetu,
Benki ya Maendeleo TIB imeunga mkono juhudi za uzalishaji wa nishati nchini kwa kutoa mkopo wa kiasi cha dola laki 4 kwa kampuni ya Nishati Lutheran (DKK) Investment Ltd inayotekeleza ujenzi wa mradi wa umeme “Ijangala Mini Hydropower” utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha kilowati 360.
Kampuni ya Nishati Lutheran (DKK) Investment Ltd inamilikiwa iliyo chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri inakusudiwa kuzalisha umeme na kuuza katika Gridi ya Taifa kupitia mradi huo.
Uzinduzi wa mradi huo umefanyika katika makao ya Kampuni ya Nishati Lutheran (DKK) Investment Ltd, yaliyopo katika kata ya Tandala, kijiji cha Msisiwe Wilayani Makete Mkoani Njombe.
Uwekaji wa jiwe la Msingi uliwekwa Askofu wa Mashariki na Pwani, Dr. Alex G. Malasusa akimuwakilisha Baba Askofu, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dkt. Fredrick Onael Shoo.
Pamoja na mkopo wa kutoka Benki ya Maendeleo TIB, mradi huo unatekelezwa kwa ruzuku kutoka kwa Wakala wa Nishati Vijini (REA) pamoja na wahisani mbalimbali wa Kanisa hilo.