Mafundi kutoka Kampuni ya Ovans Contruction Ltd inayojenga daraja katika mto Masewe Halmashauri ya wilaya Mbinga wakifanya maandalizi ya awali kwa ajili ya ujenzi wa daraja katika eneo hilo,Serikali kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)imetenga kiasi cha Sh.milioni 84 ili kufanikisha ujenzi wake.
…………………………
Na Muhidin Amri, Mbinga
SERIKALI kupitia Wakala wa barabara za mijini na vijijini(TARURA),imeanza ujenzi wa daraja katika mto Masewe linalounganisha kijiji cha Malindindo na Mikalanga katika Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma.
Meneja wa TARURA wilayani Mbinga Mhandisi Oscar Mussa alisema,serikali imeamua kujenga daraja katika eneo hilo kutokana na kuathirika vibaya na mvua za masika zilizonyesha kuanzia mwezi Disemba 2022 hadi mwezi Machi 2023.
Alisema,daraja hilo litakuwa na urefu wa mita 16 na linajengwa na kampuni ya kizalendo ya Ovans Construction Ltd kwa gharama ya Sh.milioni 84 sambamba na ukarabati wa barabara ya Mapera-Mikalanga -Ilela yenye urefu wa kilomita 16.96.
Alisema,kutokana na mvua hizo eneo hilo lilionyesha uhitaji wa kujengwa daraja kutokana na kujaa maji na hivyo kukatisha mawasiliano kwa wananchi wa maeneo hayo na hivyo kuathiri shughuli za usafiri na usafirishaji wa bidhaa.
Mussa,amewaomba wananchi kuwa na matumaini kwa kuwa ujenzi wa daraja utakamilika kwa muda wa mwezi mmoja na nusu,kutoa ushirikiano kwa mafundi na kuwa walinzi wa vifaa vya ujenzi wa daraja hilo.
Msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya Ovans Construction Ltd Frank Moyo alisema kuwa, amehaidi kazi hiyo itakamilika kwa muda uliopangwa kutokana na kampuni ya Ovans kuwa na uzoefu wa muda mrefu katika ujenzi wa madaraja na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema licha ya muda wa ujenzi kuwa mfupi,lakini daraja hilo litakuwa bora na imara na kuwaomba wananchi kuanza kujiandaa kutumia daraja hilo kwa shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali.
Baadhi ya wananchi wakiwemo wanafunzi wa shule ya Sekondari Malindindo,wameipongeza serikali kuanza ujenzi wa daraja katika eneo hilo ambalo kipindi cha masika lilikuwa halipitiki kwa urahisi kutokana na kujaa maji.
Rehema Nchimbi alisema,wakati wa masika eneo hilo ni changamoto kubwa kwani linakuwa na maji mengi yanayotoka milimani,jambo linalowaathiri sana katika masomo yao kwani wanalazimika kubaki nyumbani na hivyo kukosa vipindi darasani.
Diana Ndunguru, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa kujenga daraja,hata hivyo ameiomba Tarura kumsimamia mkandarasi kwa karibu aweze kumaliza kazi kwa muda uliopangwa ili waweze kuondokana na adha ya usafiri na usafirishaji wa mazao.