Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Serikali imesema kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) imeshiriki katika michezo mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwemo mashindano ya Dunia ya Michezo ya Majeshi yaliyofanyika Ujerumani, mwezi Julai 2022, Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Birmingham nchini Uingereza mwezi Agosti 2022, Mashindano ya Ngumi ya Ukanda wa Afrika yaliyofanyika nchini mwezi Agosti 2022, East African Championship yaliyofanyika Burundi mwezi Septemba 2022.
Aidha, mashindano mengine ni Mashindano ya Gofu yaliyofanyika Lilongwe nchini Malawi mwezi Novemba 2022, Michezo ya Majeshi (BAMMATA) iliyofanyika mkoani Mtwara mwezi Februari 2023, Mashindano ya Riadha yaliyofanyika nchini Japan 17 (Osaka Marathon) na China (Yangzhou Jianzhen International Half Marathon) mwezi Februari na Aprili 2023 mtawalia.
Akizungumza leo Mei 24, 2023 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Jujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/2024 alisema katika mashindano hayo, wanamichezo wa JWTZ waliweza kupata ushindi na kuliletea Taifa letu medali.
“Napenda kutumia fursa hii, kuwapongeza. Kipekee Sajini Taji Seleman Kidunda aliyetwaa ubingwa wa “World Boxing Federation in Africa” (WBF), Sajini Alphonce Felix Simbu, aliyepata medali ya shaba katika mbio za Osaka Marathon na Yangzhou Jianzhen International Half Marathon, Praiveti Kassim Mbudikwe na Praiveti Yusuph Changarawe, waliopata medali ya shaba kila mmoja katika mashindano ya ngumi ya Jumuiya ya Madola”. Alisema Mhe. Bashungwa.
Aliongeza “Timu teule ya mpira wa kikapu iliyoshiriki mashindano ya Majeshi Duniani yaliyofanyika nchini Ujerumani mwezi Agosti 2022 ilishika nafasi ya nne kati ya Mataifa 19 yaliyoshiriki Mashindano hayo”.