Na Eleuteri Mangi- WUSM, Johannesburg, Afrika Kusini
Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimedhamiria kuboresha na kuimarisha uhifadhi wa urithi wa ukombozi kurithisha kizazi cha sasa na vizazi vijavyo ili kuinua uchumi wa pande hizo mbili za Muungano.
Akizungumza mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa Afrika Kusini Mei 23, 2023, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi Fatma Hamad Rajab amesema kuwa Tanzania na Afrika Kusini zinahitaji kushirikiana ili kutunza urithi wake kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
“Tumekuja kujifunza namna wenzetu wanavyotunza na kuhifadhi urithi wa Ukombozi wa nchi yao na namna wanavyotunza urithi huo ili na sisi tukaboreshe maeneo yetu ya Ukombozi yaliyopo nchini kwetu’,
‘Wenzetu wamejitahidi kuweka vizuri historia yao ambayo haitaisha milele, ni kitu cha kujivunia kwa upande wao, na sisi tuna mambo mengi ya kufanya kwa viongozi wetu waasisi Mwl. Julius Nyerere na Abeid Aman Karume ambao kwetu ni urithi usiosahaulika milele kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo” amesema Bi Fatma.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Kituo cha Makumbusho cha Liliesleaf, Bw. Mosima Tokyo Sexwale amesema msaada uliotolewa na Tanzania chini ya Uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere katika ukombozi wa Afrika Kusini hautasahaulika kamwe.
“Kiukweli, misaada ya hali na tuliyopata kutoka Tanzania wakati huo ikijulikana kama Tanganyika hasa kipindi ambacho Madiba, Nelson Mandela akiwa bado anafanya harakati za ukombozi chini kwa chini, tuliomba msaada wa kisiasa, lakini tulipata zaidi ya misaada ya hali na mali pamoja na msaada wa kidiplomasia” amesema Mosima.
Mafunzo hayo ni ya siku saba kuanzia Mei 21- 27, 2023 ambapo katika siku ya pili ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Watendaji Wakuu wa Wizara hizo wamefanya ziara Johannesburg katika vituo vya Taasisi ya Makumbusho ya Nelson Mandela Foundation, kituo cha Makumbusho cha Lilieseaf ambacho kilitumiwa na wapigania uhuru wa ANC pamoja na Makumbusho yanajulikana kama Constitution Hill eneo ambalo linautajiri mkubwa wa namna mahakama zilivyofanyakazi wakati wa ubaguzi wa rangi pamoja na magereza kwa wafungwa ambao walihukumiwa kwa kesi mbalimbali.