NA MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB kwa kushirikiana na UnionPay International (UPI), wamezindua suluhisho la malipo ya kimtandao kupitia QR kwa wateja wao (NMB – UPI QR Code), huduma isiyo na mipaka ya malipo kwa watalii ama wageni wanaotua nchini kutoka Bara la Asia, wakiwemo Watanzania wanaofanya biashara kati ya Tanzania na China.
NMB – UPI QR Code, unaifanya benki hiyo kuwa ya kwanza nchini na ya tatu kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati kuwa na suluhishi hiyo chanya, ambapo mtu akiwa na ‘app’ ya UPI, ataweza kufanya malipo kwa ‘ku-scan’ kwenye QR za NMB zaidi ya 147,000 zilizopo kote nchini.
Uzinduzi huu umefanyika jijini Dar es Salaam Jumanne ya Mei 23, ukihudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo, UPI ikiwakilishwa na Meneja Mkuu wa UnionPay Tawi la Afrika, Asad Burnley, huku NMB ikiongozwa na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mponzi alisema NMB UPI QR Code unaenda kuwa chagizo la kampeni ya jamii isiyo na matumizi ya pesa taslimu na kwamba wana imani ukubwa wa taasisi hizo mbili utakuwa mhimili wa mafanikio ya bidhaa hiyo ambayo ni hatua kubwa katika kuchachua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Alifafanua kuwa, uzinduzi huo unaiongezea thamani bidhaa ya NMB Lipa Mkononi iliyo chini ya Mwamvuli wa Teleza Kidijitali, ambayo awali ilikuwa na uwezo wa kupokea Kadi za Visa na MasterCard, na kwasasa itaweza pia kuchukua Kadi ya UPI, mtandao mkubwa zaidi wa malipo unaojumuisha wateja zaidi ya Bilioni 8 duniani kote.
Mbele ya Mkuu wa Idara ya Biashara ya Kadi wa NMB, Philbert Casmir, Mponzi aliongeza: “Uzinduzi huu ni muendelezo wa ushirikiano wetu na UPI, ambao ulianza miaka miwili iliyopita, ambako ATM zetu ziliweza kupokea kadi za UPI na kutoa pesa, na sasa itakuwa hivyo kwa QR zetu zote.
“Tunajivunia mapinduzi haya ya kimtandao, ambayo yanaifanya NMB kuwa benki ya kwanza nchini kutumia UPI. Teknolojia imeifanya simu ya mkononi kuwa zana bora na muhimu, ikitumika kama njia kuu ya mhamo wa kutoka matumizi ya pesa taslimu yenye vihatarishi vingi kwenda katika ‘cashless,” alisema Mponzi.
Burney kwa upande wake alibainisha kuwa wanajivunia ujio wa bidhaa hiyo sokoni, hasa ikizingatiwa wanashirikiana na benki kubwa yenye wateja wengi zaidi nchini, miongoni mwao wakiwemo wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo pamoja na wajasiriamali wa kada hizo, ambao wanaunganishwa moja kwa moja na wateja wa UPI waliotapakaa kote duniani.
“NMB – UPI QR Code ni huduma salama, rahisi na nafuu kwa watumiaji, ambayo inaenda kuwaunganisha Watanzania na watu wa mataifa mengine 45 ya Afrika ambayo yanahudumiwa na UnionPay International.
“Tunajivunia ushirikiano huu, zaidi bidhaa hii ambayo tunaamini itakuwa chachu ya mabadiliko kwenye nyanja ya malipo kwa njia za mtandao, kwa wafanyabiashara, sekta ya utalii na wadau wake, pamoja na kampuni za kitaifa na kimataifa zinazozalisha vinywaji, vyakula na usafirishaji bidhaa za ndani na nje,” alibainisha Burney.
Shelukindo alizipongeza NMB na UnionPay International kwa ushirikiano uliozaa huduma hiyo, huku akizitaka taasisi zingine za fedha nchini kujikita katika bunifu za suluhishi za kidijitali, ambazo uhitaji wake umekuwa mkubwa Tanzania, ambako kwa takwimu za mwaka 2021 ilikuwa na laini za simu zilizosajiliwa zaidi ya milioni 54.
“Idadi hiyo kwa nchi yenye watu takribani milioni 64, inaakisi kiwango kikubwa cha mahitaji ya bunifu sahihi za kuchagiza mabadiliko katika sekta ya malipo nchini na hapa nisisitize kwamba taasisi zaidi ziongeze uwekezaji na ubunifu, kwani ukuaji kiuchumi bila pesa taslimu Tanzania, inawezekana,” alibainisha Shelukindo.