Adeladius Makwega-MWANZA
Mashindano ya Netiboli yaliyokuwa yanafanyika Kwimba mkoani Mwanza katika viunga vya Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya yamefikia ukingoni na washinfdi kukabidhiwa zawadi zao usiku wa Mei 22, 2023 na Makamu Mkuu wa Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya Alex Mkenyenge.
“Hongereni kwa kushiriki mashindano haya na walioshinda nawapa pongezi tele na ndiyo maana tunawakabidhi zawadi zenu leo hii.”
Awali jioni ya Mei 22 mashindano hayo yalianza kwa mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu ambapo uliwakutanisha Shule ya Sekondari Nyabubinza na Wanachuo cha Malya wa ngazi ya Astashahada, hadi robo zote nne za dakika 15 ambayo ni saa nzima za mchezo huu, wanachuo wa Astashahada walikuwa wameshinda magoli 32 kwa 22.
Mara baada ya mshindi watatu kupatikana, uliwadia wakati wa mbwembe na majigambo kuelekea kuanza kwa fainali iliyowakutanisha Malya Queens na Wanachuo wa Stashahada ambapo pia katika ngazi ya makundi wanachuo wa Stashahada wa chuo hiki waliwachabanga bila huruma wenyeji wao Malya Queens.
Mechi hiyo ushindani ulikuwa mkubwa sana huku ikitoa picha na uwezo wa Malya Quees iliyokuwa inaongozwa na mwalimu ambaye alisoma Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya miaka ya nyuma.
Mechi hiyo iliibua kiwewe kwa timu zote mbili ambazo sasa zilikutana fainali hiyo ya Netiboli, je hali ingekuwaje? Hapo ndipo vituko na visa vya hapa na pale viliupamba uwanja wa ndani wa chuo hiki cha umma huku meza ya Mgeni Rasmi ikipambwa na zawadi kadhaa zilizosindikizwa na sauti ya mbuzi ambaye alilia meee… meee . meee… kila mara nao mashabiki wa pande zote wakishangilia.
Walionekana mashabika hao wakifanya vituko kana kwamba wanafanya ulozi huku mashabiki wa Malya Queens ambapo waliongezewa nguvu na wanafunzi Nyabubinza Sekondari waliovalia sare zao za mashati meupe na sketi na suruali za rangi ya mgombamara baada ya kufungwa na wanachuo wa Astashahada na kuikosa nafasi ya tatu.
Mashabiki wa timu ya wanachuo wa Stashahada ya Michezo kutoka Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya walionekana wakiwa wamevalia nguo za kuchekesha wengine wakiwa wamevaa magunia, wengine walivalia nguo kama askari mgambo, mavuvuzela , filimbi na vifijo vikitawala nyuso zao zikiwa na michoro kama vikaragosi.
Timu ya Stashahada ya Chuo cha Malya kwanza ilikaguliwa huku timu wenyeji wa Malya Queens wakigoma kukaguliwana na ikionekana kuwa fainali hiyo sasa inaamuliwa kwa ushindi wa mezani. Walipouliza Malya Queens wanalalamikia nini?
“Tuna mashaka na refarii mmoja, kama wanataka tuingia uwanjani basi atafutwe refa mwingine achezeshe.”
Jambo hilo lilijadiliwa na ikaamuliwa refalii Madawa Lauzi na Lucy Malisa wauchezeshe mchezo huo. Malya Queens waliingia uwanjani na mchezo ukaanza kwa robo ya kwanza iliyokuwa na ukame wa magoli ambapo si kawaida ya mchezo wa Netiboli, mchezo huu uliendelea nazo tambo za pande zote mbili zikiendelea.
Refalii wa ndani ya uwanja Madawa Lauzi aliagiza mashabiki kupunguza kelele kusaidia wachezaji kusikia vipenga vyake alivyokuwa akivipiga uwanjani hapo kwa umahiri mkubwa, hilo lilitekelezwa na mashabiki pande zote mbili.
Magoli yalianza kungia pande zote mbili mwishoni mwa robo ya kwanza ambapo hadi robo ya nne inakamilika Malya Queens walishalala kwa magoli 33 kwa 14 tu kwa hiyo Wanachuo wa Stashahada wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya wakawa mabingwa.
Ukafika wakati wa kupokea zawadi zikiwamo fedha taslimu kwa mfungaji bora, mshindi wa tatu kutoka wanachuo wa Astashahada wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya waliopata sanduku moja la soda, Malya Queens wakiwa washindi wa pili wakipewa mpira wa Netiboli na wanachuo wa Stashahada ya Michezo Malya wakawa mabingwa wa ligi hiyo ya Netiboli wakipokea Mbuzi ambapo zawadi zote zimetolewa na mfadhili wa mashindano hayo mkufunzi Iddi Luswaga.