Serikali imekamilisha ujenzi wa jengo la kuhifadhi maiti lenye thamani ya zaidi ya mil 588 lenye uwezo wa kuhifadhi miili 36 kwa wakati mmoja katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Njombe hatua ambayo imemaliza changamoto iliyokuwa ikipigiwa kelele na wakazi wa Njombe kwa muda mrefu ya kutumia jengo la hospitali ya mji wa Njombe Kibena kuhifadhi miili ya watu wanaopoteza maisha katika hospitali ya rufaa mkoani humo.
Akiweka bayana sababu ya kutegemea jengo la hospitali ya kibena kuhifadhi maiti tangu izinduliwe julai10,2019 katibu wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Njombe Godfrey Nchia amesema ni kutokana upungufu wa majengo uliyokuwepo kipindi hicho na kwamba kuna huduma muhimu ambazo ziliendelea kutegemea hospitali ya mji kama vile kuhifadhi mahiti ,kufua nguo na kuteketeza taka.
Nchia amesema serikali imeendelea kuboresha huduma katika hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo mengine 15 uliyoanza mwezi August 2019 likiwemo la jengo la kuhifadhi maiti ambalo limekamilika lakini halijaanza kutumika kwasababu ya kukosekana kwa jenereta ambalo hadi sasa limesha agizwa.
Kuhusu changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara katika mtaa wa Wikichi na unavyokwamisha kuanza matumizi ya jengo hilo la kuhifadhi maiti katibu wa hospitali hiyo Godfrey Nchai amesema wanahofia kuanza kulitumia jengo hilo jipya kwasababu mashine ya kuhifadhi miili inahitaji umeme wa uhakika hivyo wanategemea kupokea jenereta mwezi mmoja baadae na kisha kuanza kutoa huduma hiyo.
Kwa upande wake ofisa manunuzi hospitali ya rufaa ya mkoa wa Njombe Aloyce Kavumika amesema serikali inafanya jitihada kubwa kuboresha miundombinu na huduma za matibabu katika hospitali hiyo ikiwemo ujenzi wa jengo la mochwari ,jenereta na mashine ya kuhifadhi maiti yenye uwezo wa kuhifadhi miili sita kwa wakati mmoja.
Kuhusu lini huduma ya kuhifadhi maiti itaanza kupatikana hospitalini hapo Kavumika amesema itachukua mwezi mmoja kuanza kutoa huduma hiyo na kisha kuwataka wananchi hususani wagonjwa kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kifupi.
Wakazi wa mkoa wa Njombe kutoka maeneo tofauti akiwemo Joyce Chumi na Castory Kabelege wamesema ni jambo la kushangaza kwa hospitali yenye hadhi ya rufaa kukosa jengo la mochwari hivyo wanaomba serikali iharakishe ujenzi na kisha kuanza kutoa huduma hiyo badala ya kusumbua wapendwa wao waliyopoteza maisha kuanza kusafirishwa kwenda Kibena kuhifadhiwa.
Wananchi hawa wanasema ni vyema serikali inapofanya uzinduzi wa hospitali kukawa na huduma zote za msingi kwani kukosekana kwa baadhi ya huduma kunaleta usumbufu kwa wagonjwa.