Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Mashariki, Mhe. Dkt Stergomena Tax akizungumza katika uzinduzi wa mfumo wa kuwasajili Diaspora wenye asili ya Tanzania Kidigitali (Diaspora Digital Hub) uliofanyika kwenye ukumbi wa Julius Nyerere JINCC jijini Dar es Salaam Mei 22,2023.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akimkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Mashariki, Mhe. Dkt Stergomena Tax ilikuzungumza nakuindua mfumo huo.
………………………………………….
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua rasmi mfumo wa kuwasajili Diaspora wenye asili ya Tanzania Kidigitali (Diaspora Digital Hub).
Akizindua rasmi mfumo huo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Mashariki, Mhe. Dkt Stergomena Tax (Mb.) alisema mfumo huo utasaidia Serikali kupata taarifa sahihi za Diaspora wake katika masuala mbalimbali yanayohusu Diaspora ambao ushiriki wao kwenye kujenga uchumi wa Taifa umeendelea kukua siku hadi siku.
“Mfumo huu utaisaidia Serikali kupata taarifa sahihi za Diaspora wake, utawezesha Diaspora kufahamu na kupata taarifa zinazohusu masuala mbalimbali ya Diaspora ambapo tunashuhudia ushiriki wa Diaspora katika kujenga uchumi wa Taifa letu ukiendelea kukua siku hadi siku,” alisema Dkt. Tax.
Amesema mchango wa Diaspora katika uchumi unaonekana kupitia takwimu zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania ambapo katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2021 Diaspora walituma nchini Dola za Marekani Milioni 569.3 na mwezi Januari hadi Desemba 2022 walituma nchini kupitia vyanzo rasmi Dola za Marekani Bilioni 1.1 ambazo ni sawa na Shilingi Trilioni 2.6.
Aliongeza kuwa Diaspora hao kwa mwaka 2021 walinunua nyumba na viwanja nchini zenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.3 na mwaka 2022 walitumia Shilingi Bilioni 4.4 kununua Nyumba na Viwanja nchini.
Alisema Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (UTT-AMIS), unaonesha kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba 2022 Diaspora waliwekeza Shilingi Bilioni 2.5 katika mifuko mbalimbali ya UTT- AMIS.
Awali akizunguma katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge – Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa (Mb), alisema kuuanzishwa kwa mfumo wa kuwatambua Diaspora wenye asili ya Tanzania ni jambo muhimu litakaloiwezesha Serikali kupata taarifa sahihi za Diaspora wake.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo alitoa wito kwa Diaspora wautumie Mfumo huo ili kuiwezesha Serikali kupata kanzidata itakayoiwezesha kupanga mipango mbalimbali na kuwawezesha Diaspora kupata fursa zilizopo nchini.
“Zaidi ya kuiwezesha Serikali na Taasisi Binafsi na za Umma kupata takwimu sahihi za idadi ya Diaspora wa Tanzania Kidigitali, Mfumo wa DDH utakuwa na faida nyingi ikiwemo, Kukusanya Kidigitali taarifa za Diaspora kama vile taarifa kuhusu jinsia, elimu na Utaalam na Kuwawezesha Diaspora kushiriki kidigitali katika shughuli mbalimbali za Maendeleo, Biashara, Uchumi na Uwekezaji, kupitia Taasisi za Biashara, Uwekezaji na Huduma zitakazokuwa zimesajiliwa katika Mfumo huo,” alisema Dkt. Shelukindo
Dkt. Shelukindo alifafanua kuwa mfumo huo utawawezesha Diaspora kupata huduma maalum zinazopatikana kupitia Mfumo huo, ambazo zitakidhi mahitaji yao kama vile huduma za Kibenki; Hifadhi ya Jamii; fursa za Uwekezaji, Biashara na Masoko; masuala ya Uhamiaji; Vitambulisho vya Taifa na huduma nyinginezo muhimu ambazo zitafikiwa kwa urahisi kupitia Mfumo huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Bw. Abdulmajid Nsekela, alieleza faida za mfumo huo kuwa ni kuwawezesha Diaspora kufungua akaunti, pia kadi zote za CRDB zimeunganishwa na mfumo, mfumo pia umeunganishwa na mfumo wa kukusanya mapato yake yasiyo ya kodi kwa kidijitali (GePG) na kuwezesha Diaspora kutambua kwa urahisi fursa za uwekezaji nchini.
Naye Mwakilishi wa Mkuregenzi Mkuu wa Benki ya NMB, Bw. Philbert Mponzi alisema Benki ya NMB kupitia mfumo huo imeanzisha dawati maalumu la kuwahudumia Diaspora kwa ukaribu zaidi.
Mkurugenzi Mkuu Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba alisema NSSF itaendelea kuunga mkono mfumo huo na wataendelea kushawishi diaspora kujiunga na mfumo huo na kujiunga na mfumo wa hiari wa hifadhi ya jamii kwa faida ya maisha yao ya uzeeni.
Mkurugenzi Mkuu Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba
Mwakilishi wa Mkuregenzi Mkuu wa Benki ya NMB, Bw. Philbert Mponzi akizungumza kwa upande wa wafadhili wa ujezi wa mfumo huo wa kidijitali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge – Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa (Mb)
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI), Dk Anna Makakala