Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip
Mpango leo tarehe 22 Mei 2023 amewasili katika mji wa Sharm El
Sheikh nchini Misri ambapo anatarajia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika
Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
unaofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 26 Mei 2023.
Mkutano huo unajumuisha Mkutano wa Mwaka wa Baraza Kuu la Benki
ya Maendeleo ya Afrika na Mkutano wa 49 wa Mfuko wa Maendeleo ya
Afrika chini ya kauli mbiu ya “Kuhamasisha Ufadhili wa Sekta Binafsi
kwaajili ya Maendeleo ya Kijani Barani Afrika”
Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo utajadili namna Afrika
inavyoweza kutumia sekta binafsi katika kutekeleza ajenda ya
mabadiliko ya tabianchi ili kufanikisha lengo lake la maendeleo jumuishi
ya kijani.
Mkutano huo unahudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali, Mawaziri wa
Fedha, Magavana, Viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Kimataifa,
Sekta Binafsi pamoja na Wawakilishi kutoka Asasi za Kiraia.
Franco Singaile
Msaidizi wa Makamu wa Rais – Habari