Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha,Profesa Eliamani Sedoyeka akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo jijini Arusha.
Afisa Uhusiano chuo cha uhasibu Arusha (IAA),Sarah Goroi akitoa elimu kwa wadau mbalimbali waliotembelea banda hilo katika maonesho jijini Arusha .
……………………………………
Julieth Laizer,Arusha .
Chuo cha uhasibu Arusha (IAA) kupitia kituo cha kiatamizi kinacholenga kuwajengea uwezo vijana wa chuo hicho kukuza mawazo yao ya biashara kimewekeza kiasi cha shs milioni 700 kwa ajili ya kusaidia vijana hao.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha, Profesa Eliamani Sedoyeka wakati akizungumza katika maonesho ya mafunzo ya ufundi Stadi yanayofanyika katika viwanja vya Stadium jijini Arusha.
Profesa Sedoyeka amesema kuwa,fedha hizo zimetumika katika kuandaa kituo hicho sambamba na kutenga kiasi cha shs milioni 100 kwa ajili ya kuwawezesha vijana mitaji kwa ajili ya kuendeleza biashara zao .
Amesema kuwa ,kituo hicho kina malengo mbalimbali ya kuwatafutia mitaji,kuboresha uzalishaji,kuwasaidia kupata masoko ya uhakika na hatimaye kufikia kampuni.
Ameongeza kuwa,kitendo cha kuwaandaa vijana wao kinawasaidia wao kuweza kujiajiri na kuajiri wengine huku kampuni zao zikizidi kukua na kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwa ni kuunga mkono lengo la kujenga Tanzania ya viwanda ambapo kituo kimejipanga kukuza zaidi ya biashara 40 kwa wakati mmoja.
Amefafanua kuwa,vijana wenye wazo la biashara wameweza kuwasaidia kuwa wazo la makampuni ambapo kwa mwaka huu wamewawezesha vijana hao kuanzisha makampuni 6 .
“Tunachotaka sisi ni kuhakikisha wanafunzi wakihitimu wanakuwa watengeza ajira na sio watafuta ajira na hii inasaidia sana kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira iliyopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini “amesema.
Amesema kuwa , wizara imekuwa ikifanya vuzuri sana katika kurekebisha mitaala mbalimbali ambayo itasaidia vijana kujiajiri na wamekuwa wakishirikiana na wizara kwa karibu sana katika maswala hayo .
Aidha ameongeza kuwa,kwa mwaka huu chuo hicho kimeweza kuanzisha kozi mpya ya bachelor degree ambayo imewezesha kuzalisha wataalamu wa kutosha ,ambapo amewataka vijana waliohitimu kidato cha sita ndio muda wa kuchangamkia fursa hiyo kwa kujifunza kozi mbalimbali chuoni hapo.
“Sisi tumejipanga kwa kutoa kozi za kimkakati ikiwemo ya uanagenzi katika maswala ya bima,na utalii ambapo wanafunzi wetu wamekuwa wakiandaliwa vizuri na kupata muda mzuri wa kujifunza zaidi.”amesema Profesa Sedoyeka .