MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesema kufuatia changamoto ya Wanyamapori Wakali na Waharibifu inayokabili Wilaya ya Mvomero, Serikali imechukua hatua mbalimbali mahsusi katika kuhakikisha inapunguza changamoto hiyo kwa wananchi.
Hayo yamesemwa Mei 19, 2023 Wilayani Mvomero na Mhifadhi Gilbert Magafu akitoa wasilisho katika warsha ya kujadili utatuzi wa changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu inayoikabili Wilaya hiyo, warsha iliyoratibiwa na TAWA.
Mhifadhi Gilbert amesema kwa kutambua ukubwa wa Wilaya ya Mvomero ikilinganishwa na ukubwa wa changamoto ya wanyamapori hao, Serikali imesogeza huduma Kwa wananchi kwa kugawa maeneo ya kufanyia kazi kwa taasisi za TAWA na TANAPA.
Akitolea ufafanuzi mgawanyo huo amesema, TAWA inawajibika moja kwa moja kuhudumia kata nane (8) ambazo ni Rubungo, Melela, Mlali, Dakawa, Songaji, Mvomero, Kanga na Homboza wakati TANAPA ikiwajibika kuhudumia kata tatu (3) ambazo ni kata ya Doma, Msongozi na Mangae.
Katika kudhibiti wanyamapori hao, Gilbert amesema katika kipindi cha Julai 2021 hadi Aprili 2023 TAWA imefanikiwa kudhibiti jumla ya matukio 311 ya wanyamapori wakali na waharibifu kwa kufanya doria za mara Kwa mara zilizofanywa na askari wa Mamlaka hiyo.
Sanjari na kazi za doria, elimu ya uhifadhi kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi imepewa kipaumbele ili kuwasaidia wananchi kuwa na uelewa wa tabia za wanyamapori na elimu ya mbinu rafiki za kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao.
“TAWA kupitia kitengo cha ujirani mwema katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Mei 2023 tumefanikiwa kutoa elimu ya uhifadhi kwa watu 4,129 kwenye vijiji 23 na shule 9” amesema.
Kwa upande wake Afisa Mhifadhi kutoka TAWA, Isaac Chamba amesema kutokana na wanyamapori hao kuonesha hali ya kuhatarisha maisha ya watu na mali zao, TAWA ililazimika kuwavuna baadhi ya wanyamapori hao ili kuokoa maisha ya watu.
“Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Aprili 2023 tulilazimika kuvuna jumla ya tembo wakorofi 7 kwa ajili ya kuimarisha usalama wa maisha ya watu na mali zao katika Wilaya hii ya Mvomero ” amesema.
Aidha jitihada nyingine zilizofanywa na Serikali kupitia TAWA ni pamoja na kusambaza kwa wananchi namba za kupiga simu bure na za wakuu wa vituo ambapo jumla ya mabango 262 na vipeperushi 500 vyenye namba hizo vimesambazwa katika kata 8 na vijiji 23 vya Wilaya ya Mvomero.
Pia, zoezi la kugawa mbegu za pilipili, kuanzisha vikundi vya ulinzi wa mazao na kutoa vifaa vya kufukuzia tembo zimekuwa ni sehemu ya jitihada endelevu za Serikali katika kuhakikisha changamoto ya wanyamapori hao inapungua katika Wilaya hiyo.
Aidha, mikakati mbalimbali inayoendelea kutekelezwa hadi sasa ni pamoja na kuendelea kuajiri askari wahifadhi, kuongeza vitendea kazi, kushirikiana na TAWIRI katika kufanya tafiti ikiwemo kuvalisha “GPS Satellite Collars” kwa makundi ya tembo.
Pia, kushirikisha askari wanyamapori wa vijiji (VGS) katika doria za kudhibiti wanyamapori hao kwenye maeneo korofi pamoja na kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi ya nadharia na vitendo.