Na John Mapepele
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka watendaji wa sekta ya Misitu na Nyuki kukamilisha mkakati wa kuongeza uzalishaji wa asali toka tani 35000 za sasa hadi tani 138000 katika kipindi cha miezi miwili alioupa jina la mkakati wa “achia shoka kamata mzinga” huku akitaka eneo la misitu na asali kufanyiwa utafiti wa kutosha ili litumike kama zao jipya la utalii.
Mhe Mchengerwa ameyasema hayo leo Mei 21, 2023 wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Uwanja wa Bombadia mkoani Singida.
Akiwa kiwanjani hapo amezindua Mwongozo wa Usimamizi wa Hifadhi za nyuki, na vibanda maalum vya kuuzia asali pia ametoa Tuzo 5 za wadau wenye mchango mkubwa kwenye Sekta ya nyuki na ametoa vyeti kwa wanafunzi walioandika nsha nzuri kuhusu ufugaji wa nyuki.
Akisoma hotuba yake amesema pamoja na uwepo wa maeneo makubwa yaliyohifadhiwa na yanayofaa kwa ajili ya kuzalisha mazao ya nyuki yenye viwango bora vado takwimu zinaonesha uzalishaji ni 23% ikilinganishwa na uwezo uliopo wa kuzalisha tani 138,000 kwa mwaka.
Kutokana na hali hiyo Mhe. Mchengerwa ameelekeza Wizara ya Maliasili ishirikiane na Wizara ya Kilimo kuanzisha programu za matumizi ya makundi ya nyuki kwenye uchavushaji mimea ili tuweze kuongeza kiwango na ubora wa mazao yanayozalishwa.
Ameitaka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mfuko wa Misitu kuhakikisha wanawezesha wananchi hasa wale wanaopakana na maeneo ya hifadhi kwa kuwapatia mafunzo ya ufugaji nyuki pamoja na mizinga ya kisasa. Pia kushirikiana na wadau mbalimbali kuhamasisha jamii kupanda na kuitunza miti katika maeneo yao.