Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Diwani wa kata ya Nyakabango Wilayani Muleba Mkoani Kagera Mhe. Pastory Gwanchele ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Afya kwa Ujumla kwa kuhakikisha elimu ya afya kwa umma dhidi ya mlipuko wa magonjwa na masuala ya lishe inafika kila mahali ikiwemo mjini na vijijini.
Mhe. Gwanchele amebainisha hayo mara baada ya timu ya watalaam wa afya kutoka mkoa wa Kagera, Wizara ya Afya pamoja na wadau kufika katika zahanati ya Katembe na kuzungumza na watumishi wa afya katika zahanati hiyo kujionea namna elimu ya afya inavyotolewa katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
“Ndugu wataalam nawashukuru sana jinsi mnavyofanya jitihada kujikinga na magonjwa ya mlipuko ,magari yamefika maeneo ya kata yote ndani kabisa vijijini elimu ya afya imetolewa na inaendelea kutolewa ,naishukuru sana Wizara ya Afya kupitia kwa Mhe.Ummy Mwalimu ,vilevile ninamshukuru Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan tukiangalia sisi mkoa wa Kagera mlipuko ulitokea lakini sasa ni salama”amesema.
Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoa wa Kagera Zablon Segeru ametumia fursa hiyo kuiasa jamii kuendelea kuchukua tahadhari zaidi dhidi ya magonjwa ya mlipuko.
“Cha msingi zaidi nasisitiza zaidi jamii kuendelea kuchukua tahadhari za haya magonjwa ya mlipuko mimi niwashukuru kwa hii kamati ya serikali ya Kijiji kwa namna ambavyo wanaendelea na mikakati mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu yao vizuri hasa katika masuala ya elimu ya afya”amesema.
Akizungumza na watumishi wa Afya katika Zahanati ya Katembe Mtaalam wa Afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Jackline Saulo amewaasa watumishi hao kuwa na mpango kazi endelevu katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
“Tuwe na Mpango kazi endelevu katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ili tuwalinde wananchi wetu, lazima tutoe elimu mara kwa mara mfano desturi ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni iwe desturi “amesema.
Afisa Lishe Mkoa wa Kagera Joanitha Jovin pamoja na Mratibu Elimu ya Afya Halmashauri ya Muleba Grace Nkonjelwa wametumia fursa hiyo kuweka msisitizo zaidi kipaumbele cha elimu ya afya pindi huduma zinapotolewa.
Halikadhalika, timu ya watalaam wa afya ilifika katika mwalo wa Katungulu na kutoa elimu ,vipeperushi na mabango ambapo Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoa wa Kagera Zablon Segeru alihimiza umuhimu wa kuzingatia kanuni za Afya ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa vyoo bora, kunawa mikono mara kwa mara kuepuka magonjwa ya mlipuko.
Ikumbukwe kuwa katika Zahanati ya Katembe zaidi ya watumishi 10 walikumbushwa umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya afya huku mwalo wa Katunguli katika boti iliyokuwa ikielekea Mlumo abiria 18 na jumla ya watu 26 waliweza kukumbushwa umuhimu wa kuzingatia kanuni za afya katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.