Julieth Laizer,Arusha.
Wanawake wametakiwa kujitokeza kwa wingi kusomea kozi za uongozaji wa meli ili waweze kunufaika na fursa zote na kuweza kupata ajira kwa urahisi.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha Mhadhiri Msaidizi wa chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI),Azan Juma Azan wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha katika Maonesho ya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi yanayofanyika jijini Arusha.
Azan amesema kuwa, uwiano uliopo chuoni hapo kati ya wanawake na wanaume bado idadi ya wanawake ni ndogo ikilinganishwa na wanaume na hiyo ni kutokana na dhana iliyokuwepo ya kuwa kozi hiyo ni kwa ajili ya wanaume tu.
“Ila kwa sasa hivi tunashukuru mwitikio wa wanawake kujiunga na kozi zetu umeanza kuonekana kwani idadi ya wanawake inaendelea kuongeza siku hadi siku na tunaendelea kutoa elimu zaidi ili idadi hiyo niendelee kuongezeka zaidi”amesema Azan.
Amesema kuwa chuo hicho kimekuwa kikiwaandaa watalaamu bora na waliobobea kwani ni chuo pekee Tanzania na Afrika Mashariki na kati kimepata hiyo idhibati.
Ameongeza kuwa, chuo hicho kinatoa kozi za uongozaji wa meli,uhandisi wa meli ,uongozaji wa mzigo,usimamizi na uchimbaji wa mafuta gesi,wasanifu,sheria za habari,uchimbaji wa mafuta na gesi pamoja na kufanya ukaguzi wa vifaa vyote vinavyotumika kwenye meli kwa ajili ya uokozi.
Amesema kuwa, changamoto ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo ni jamii kuchukulia kozi ya Baharia kama uhuni, huku akiwataka kufahamu kuwa Baharia ni mtu yoyote anayefanya kazi ndani ya meli na ni lazima awe na taaluma au ujuzi wa kufanya kazi hiyo.
“Tumefungua dirisha la usajili kwa ngazi ya cheti hadi diploma kwa dirisha la masomo Septemba hivyo tunatoa rai kwa watu mbalimbali wajitokeze kwa wingi .”amesema.
Naye Mmoja wa wanafunzi ,Wilfrida Ngallu mwanafunzi wa mwaka wa 4 katika shahada ya uhandisi wa meli na vifaa vya madini,amesema kuwa,pamoja na kuwa watu wanachukulia kozi hiyo kama kozi ya wanaume peke yake lakini yeye amedhubutu kusomea kwani ana shauku kubwa ya kusafiri duniani .
“Mimi nimeamua kujikita kwenye sekta hii kwani ni sekta inayolipa sana kutoka na kuwepo kwa fursa nyingi kutokana na serikali kuweka jitihada zaidi ,hivyo nawashauri wasichana wajitokeze kwa wingi kusomea kozi hiyo kwani wataweza kujifunza mambo mengi sana ambayo yatawafikisha mbali.”amesema.