Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya maadili ya wanasheria wakifuatilia mafunzo hayo yaliyofanyika Ukumbi wa Zssf Kariakoo Mjini Unguja,Mei 20,2023.
Jaji wa Rufaa Tanzania dkt.Gerald Ndika alipokuwa akiwasilisha mada ya Maadili ya Maafisa wa mahakama kwa wadau wa sheria wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya maadili ya wanasheria yaliyofanyika Ukumbi wa Zssf Kariakoo Mjini Unguja,Mei 20,2023.
Rais wa jumuiya ya mawakili Zanzibar Slim Said Abdalla akifanya mahojiano na waandishi wa habari kuhusiana na maadili ya wanasheria wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa wadau wa Sheria yaliyofanyika Ukumbi wa Zssf Kariakoo Mjini Unguja,Mei 20,2023.
Rais wa Wanafunzi wa Skuli ya Sheria Zanzibar Sleimani Mrisho akifanya mahojiano na waandishi wa habari kuhusiana na maadili ya wanasheria wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa wadau wa Sheria yaliyofanyika Ukumbi wa Zssf Kariakoo Mjini Unguja,Mei 20,2023. PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR.
Na Fauzia Mussa -Maelezo
Wanasheria, Majaji na Mahakimu wametakiwa kuwacha maslahi binafsi wakati wanapofanya kazi zao na badala yake kufuata miiko na maadili ya sheria ili kuhakikisha haki inapatikana.
Akifungua mafunzo ya kuwajengea uwelewa juu ya maadili ya wanasheria wanafunzi wa Skuli ya Sheria huko Ukumbi wa Zssf Kariakoo Mjini Unguja Mwenyekiti wa Baraza la Skuli ya Sheria Zanzibar Mbarouk Salim Mbarouk amesema, bila ya kufuata maadili jamii haitakua na kimbilio la kupata haki zao hivyo amewataka mafisa hao kufuata maadili kwani ndio msingi bora wa utendaji wa kazi.
Aidha alifahamisha kuwa kazi ya uhakimu ni kazi ngumu na yenye dhima hadi kwa mungu hivyo amewaomba watendaji hao kutokuwa na upendeleo wakati wanapohukumu kwa maslahi binafsi.
Alieleza kuwa si kila mtu anaweza kuhukumu hivyo ni lazima mtu asomee fani hio na awe tayari kufuata maadili ya wanasheria ili kuisaidia jamii kupata haki zao.
“kufanya kazi za sheria ni kama unafanya kazi ya mungu tujitahidi kutenda haki ukizingatia ipo siku na wewe utahukumiwa kutokana na hukumu uliyomuhukumu mwengine “alisisitiza Mwenyekiti huyo.
Alieleza kuwa kwa kipindi kirefu sasa jamii imekuwa ikiwalalamikia watendaji wa sheria juu ya utendaji wa kazi zao hivyo mafunzo hayo yana lengo la kuwaiimarisha na kuwawezesha watendaji hao kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Mwenyekiti huyo amesema mafunzo hayo yameelekezwa kwa skuli ya sheria kwani hapo ndio eneo la kuwapika na kuwaandaa mawakili,majaji na wanasheria hivyo amewaomba washiriki hao kuyafanyia kazi mafunzo hayo ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa.
Kwa upande wao washiriki wa Mafunzo hayo wameahidi kuyafanyia kazi na kuhakikisha wanatenda haki wakati wakitekeleza majukumu yao ya kila siku.
Katika mafunzo hayo yaliyowashirikisha wadau mbali mbali wa Sheria mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwemo Maadili ya Maafisa wa mahakama , na maadili ya mawakili wa umma na wakujitegmea.