Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke, Mhandisi Jahulula M. Jahulula akizungumza leo tarehe 19/5/2023 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam akiwa katika Operesheni ya ukaguzi miundombinu ya TANESCO pamoja kuwatembelea wateja kwa ajili ya kutatua changamoto katika Kata ya Kurasini, Mtaa wa Tumbaku Klabu.
Afisa Usalama Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Stephen Maganga akifafanua jambo akiwa katika ukaguzi wa miundombinu ya TANESCO katika Kampuni ya Royal Recycling Limited inayonzalisha mifuko ya Plastic iliyopo Kata ya Kurasini jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke wakifanya ukaguzi wa miundombinu ya Shirika hilo katika Kampuni ya Royal Recycling Limited iliyopo Kata ya Kurasini jijini Dar es Salaam.
Mfanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke akikata umeme katika Kampuni ya Royal Recycling Limited iliyopo Kata ya Kurasini jijini Dar es Salaam baada ya kubainika wanatumia umeme bila mita (umeme wa wizi).
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
…….
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke kupitia Operesheni ya ukaguzi pamoja na kuangalia miundombinu yake wamefanikiwa kumkamata mteje wao Bw. Jimmy Amani mmiliki wa kampuni ya Royal Recycling Limited kwa tuhuma ya kutumia umeme bila mita jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Kampuni hiyo ya Royal Recycling Limited inanzalisha mifuko ya Plastic inayopatikana Kata ya Kurasini, Mtaa wa Tumbaku Klabu ambapo TANESCO Mkoa wa Temeke walikuwa wanaendelea na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza leo tarehe 19/5/2023 Jijini Dar es Salaam akiwa Operesheni ya ukaguzi pamoja na kuangalia miundombinu katika Kata ya Kurasini, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke, Mhandisi Jahulula M. Jahulula, amesema kuwa mmiliki wa Kampuni ya Royal Recycling Limited Bw. Amani wamemkuta anatumia umeme wa TANESCO asilimia 100 bila kutumia mita.
Mhandisi, Jahulula amesema kuwa utaratibu wa kumchukulia hatua unaendelea ikiwemo kumkatia umeme pamoja na kukamatwa na vyombo vya dola kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mhandisi Jahulula ameeleza kuwa Operesheni hiyo ni endelevu na sehemu ya majukumu yao ya kila siku katika kuhakikisha wanawatembelea wateja ili kutatua changamoto pamoja na kukagua miundombinu ya TANESCO.
Aidha Afisa Usalama Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Stephen Maganga, amesema kuwa wizi wa umeme unarudisha nyuma jitihada za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassani katika kutoa huduma kwa wananchi kupitia TANESCO.
Bw. Maganga amesema kuwa mtu akitumia umeme bila kulipa mapato ya Shirika yanapotea, huku akitoa wito kwa watanzania kuwa wateja wenye uweledi ili jitihadi za kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma ya umeme inafikiwa.
Mhandisi kutoka Kanda ya Mashariki, Mrisho Sangiwa, amesema kuwa kutumia umeme bila kufata utaratibu ni hatari kubwa ambayo ingeweza kusababisha moto katika eneo hilo.
“Mteja wetu aliunga wire kwenda katika mashine za kuzalisha bidhaa zake bila kufata utaratibu hivyo usalama mali pamoja na binadamu ulikuwa katika mashaka makubwa” amesema Mhandisi Sangiwa.
TANESCO Mkoa wa Temeke wamejipanga kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake sambamba na kuwasaka wateja wote wanao hujumu miundombinu yake ya umeme.