Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amekemea vikali tabia ya wananchi wa Wilaya hiyo kuwajeruhi wanyama tembo akidai kuwa vitendo hivyo huamsha hasira Kwa wanyama hao na hatimaye kuwaletea madhara
Ameyasema hayo Mei 19, 2023 wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro katika warsha ya kujadili utatuzi wa changamoto ya Wanyamapori Wakali na Waharibifu inayoikabili Wilaya hiyo, warsha iliyoratibiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA)
“Nimepata taarifa kwamba Kuna watu wanachokoza wanyama, mtu anajeruhi tembo, tembo ukishamjeruhi tayari anakuwa na hasira lazima asumbue hicho Kijiji kwasababu ana maumivu ” amesema
“Nimepata taarifa Kuna baadhi ya tembo wanakutwa wakiwa na madonda, hata wakimkamata wanakuta tayari anavuja usaha, Sasa tembo wa namna hii haiwezi kuwa rahisi kumzuia lazima atakufanyia fujo kwasababu ana maumivu” ameongeza
Mhe. Judith amekemea pia vitendo vya wananchi kufanya shughuli za kibinadamu pembezoni mwa hifadhi kama vile kilimo jambo ambalo linawapelekea tembo kuharibu mazao yao.
“Tunaona kabisa hifadhi hii, mtu analima pembeni hii ni Changamoto kwasababu yule mnyama akitoka tu anakumbana na hilo Shamba, lazima aliathiri kwasababu mnyama ni mnyama tu hana akili za kujua hili ni Shamba nilikwepe” amesema
Kwa Upande wake Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi TAWA Mlage Kabange amesema tathmini iliyofanywa na TAWA katika maeneo mbalimbali Nchini imebaini kuwa watu wengi wanaopata madhara yanayotokana na Wanyamapori Wakali na Waharibifu hususan tembo yanatokea Wakati wa alfajiri na usiku, hivyo ametoa rai kwa wananchi kuepuka kufanya matembezi yasiyo ya lazima nyakati za Usiku na alfajiri.
Mlage Kabange amesema katika Kukabiliana na changamoto hiyo, TAWA imejenga kituo cha Askari Kwa ajili ya muitikio wa haraka Ili kuweza kuwadhibiti Wanyama Wakali na Waharibifu kilichopo katika Kijiji Cha Sangasanga na amewaomba viongozi wa Kijiji kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza wananchi kukutumia kituo hicho Kwa kutoa taarifa za matukio ya uvamizi wa Wanyama hao
Naye mbunge wa Jimbo la Mvomero Jonas Van Zeland ameziomba mamlaka zinazohusika na Wanyamapori hususan TAWA kuwavuna tembo Kwa lengo la kuwapunguza Ili kuwapunguzia wananchi adha wanayokumbana nayo.
Warsha hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Serikali ambapo ilihusisha viongozi mbalimbali katika Wilaya hiyo wakiwemo Ku ya Wilaya, madiwani wa kata, wenyeviti na watendaji wa kata, watendaji wa vijiji, wawakilishi wa Wazee Wote kutoka katika Wilaya ya Mvomero
Mawasilisho mbalimbali yaliwasilishwa Kwa lengo la kuwapatia elimu viongozi hao
Mojawapo ya mawasilisho hayo ni njia rafiki za kupambana/kudhibiti Wanyamapori Wakali na Waharibifu, Utaratibu wa kifuta jasho/machozi Kwa wananchi, mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Wanyamapori Wakali na Waharibifu pamoja na hali ya tatizo la Wanyamapori Wakali na Waharibifu katika Wilaya ya Mvomero na hatua zinazochukuliwa na TAWA