Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Janeth Haule akitoa taarifa ya utendajikazi wa Taasisi yake kwa wanahabari katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi 2023
…………………………………….
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa
Ruvuma imebaini mapungufu katika utekelezaji wa miradi mitano ya
maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5.5.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma katika
kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi 2023 kwa wanahabari,Naibu Mkuu
wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Janeth Haule,amesema hatua
mbalimbali zilichukuliwa ili kuondoa mapungufu hayo kwenye miradi hiyo.
Hata hivyo amesema katika kipindi hicho TAKUKURU ilifuatilia utekelezaji
wa miradi 15 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6.5.
Ameitaja miradi iliyobainika kuwa na mapungufu kuwa ni mradi wa ujenzi
wa madarasa tisa katika shule ya sekondari Sasawala wilayani Namtumbo
wenye thamani ya shilingi milioni 180,ambapo TAKUKURU ilibaini mradi
kuchelewa kukamilika kutokana na ucheleweshaji wa ununuzi wa vifaa na
mafundi.
“TAKUKURU tulitoa ushauri kwa Halmashauri kutoa ukomo wa bei kwa
wazabuni na kufanya malipo kwa wakati baada ya kujiridhisha na
uchunguzi’’,alisisitiza Haule.
Kulingana na Naibu Mkuu wa TAKUKURU,ameutaja mradi mwingine
waliobaini mapungufu kuwa ni ujenzi wa majengo matatu katika hospitali ya
wilaya ya Namtumbo unaogharimu shilingi milioni 800,ambapo walibaini
mradi kuchelewa kukamilika ambapo TAKUKURU ilishauri kufanya
tathimini sahihi ya vifaa na kufanya manunuzi ya jumla.
Haule ameutaja mradi mwingine waliobaini mapungufu ni ujenzi wa jengo
la wagonjwa wa nje (OPD) katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea
unaogharimu shilingi bilioni 3.87 ambapo TAKUKURU ilibaini kuchelewa
kukamilika kwa mradi, ucheleweshaji wa makabidhiano na mradi kufanyika
kwa awamu mbili.
Amesema TAKUKURU ilishauri kukamilishwa haraka kwa mradi huo katika
awamu ya pili ili kuepuka upotevu wa vifaa vya ujenzi kutokana na kurudia
kazi moja mara mbili.
Miradi mingine iliyogundulika kuwa na mapungufu ni ujenzi wa hospitali ya
wilaya ya Mbinga unaogharimu shilingi milioni 500 na ujenzi wa kituo cha
afya Kata ya Mbangamao Mbinga unaogharimu shilingi milioni 250.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma amesema katika kipindi
hicho TAKUKURU ilipokea malalamiko 20 kati ya hayo malalamiko tisa ni
ya rushwa na kwamba TAKUKURU iliweza kutoa elimu kupitia semina
26,klabu za wapinga rushwa 70 za shule za msingi na sekondari,mikutano
ya hadhara 11,vipindi vya redio vinne,Makala saba na maonesho saba.