Julieth Laizer,Arusha .
Jumla ya vijana 43,000 wamenufaika na Mfuko wa kuendeleza ujuzi(SDF) unaoratibiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) unaolenga kuwezesha Taasisi zinazotoa mafunzo kuongeza ubora na ufanisi katika kutoa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi katika sekta sita za kipaumbele nchini.
Aidha Mfuko wa SDF ni sehemu ya Programu ya kuendeleza Elimu ya Ujuzi na Mafunzo ya Stadi za kazi zenye kuleta tija katika ajira na mpango mkakati wa kitaifa wa kukuza na kuendeleza ujuzi nchini.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Afisa habari wa TEA,Eliafile Solla wakati akizungumzia kuhusiana na mfuko huo katika Maonesho ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi yanayofanyika kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Solla amesema kuwa, mfuko huo unawawezesha vijana kuendeleza ujuzi wao na uwezo wa kujishughulisha na shughuli za kiuchumi ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine .
Amesema kuwa,Mfuko huo unatoa ufadhili kwa Taasisi zinazolenga kutoa mafunzo ya kuendeleza ujuzi katika sekta sita za kipaumbele zinazoratibiwa na Programu ya ESPJ ambazo ni kilimo na kilimo uchumi,utalii na huduma za ukarimu,uchukuzi,ujenzi ,Teknolojia ya habari na Mawasiliano (TEHAMA)pamoja na Nishati .
Aidha ameongeza kuwa,mfuko wa SDF unasimamia programu za ESPJ ambazo ni Utarajali na Uanagenzi,kujenga uwezo wa Taasisi za mafunzo,mafunzo ya kiubunifu na elimu mtandao,mpango wa ufadhili kwa vijana wanaotoka kaya maskini na wanaoishi katika mazingira magumu.
Amefafanua kuwa, mfuko huo unatoa ruzuku kwa Taasisi zinazotoa mafunzo nchini katika ngazi nne kwa kuzingatia madaraja ya mafunzo .
Solla ameongeza kuwa,mradi wa SDF hutekelezwa ndani ya mwaka mmoja ambapo Taasisi nufaika inatakiwa kuendesha mafunzo mafupi ya mwezi mmoja hadi miezi mitatu kwa makundi tofauti hadi kufikia idadi ya wanufaika iliyowekwa kwa Taasisi husika.
Amesema kuwa, kupitia mfuko huo vijana wengi wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani wameweza kujiajiri na wengine kutengeneza ajira kwa wengine na hivyo kuondokana na changamoto ya ajira iliyopo nchini.