Na Shamimu Nyaki.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana leo Mei 17, 2023 ameongoza kikao cha Mawaziri wanaohusika na Michezo wa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ambao ni Mhe. Peter Ongwang wa Uganda na Ababu Namwamba wa Kenya kujadili maandalizi ya pamoja ya mashindano ya Kombe la Africa Cup of Nation (AFCON) mwaka 2027.
Kikao hicho ambacho kimefanyika kwa njia ya mtandao kimejadili namna nchi hizo zinavyoweza kushirikiana kuandaa mashindano hayo kupitia mashirikisho ya mipira ya nchi hizo.
Mawaziri wamewasisitiza kikosi kazi kilichoteuliwa, kuandaa mpango kazi wenye ushawishi kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kabla ya Mei 2023 ili nchi hizo zipate nafasi ya kuandaa mashindano hayo.
Kwa upande wa Tanzania Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu ameshiriki pamoja na Viongozi wa Mashirikisho ya Mpira wa Miguu ya nchi hizo, ambapo kwa Tanzania imewakilishwa na Bw. Boniface Wambura kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).