Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi hiyo katika hafla fupi ya kuwapongeza madaktari bingwa wa moyo waliokwenda kutoa huduma za upimaji na matibabu katika Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpongeza Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi hiyo Dkt. Angela Muhozya pamoja na timu ya wataalamu wa Taasisi hiyo waliokwenda nchini Malawi katika Hospitali ya Queen Elizabeth kwaajili ya kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza katika hafla fupi ya kuwapongeza madaktari bingwa wa moyo waliokwenda kutoa huduma za upimaji na matibabu katika Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi.Picha na JKCI.
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itaendelea kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa nchi zinazoizunguka Tanzania ili huduma hiyo iweze kuwafikia watu wengi zaidi na kuokoa maisha yao.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza madaktari bingwa wa moyo waliokwenda kutoa huduma za upimaji na matibabu katika Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi.
Dkt. Kisenge alisema Taasisi hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka nchi za Afrika ya Mashariki na Kati ikiwemo Malawi lakini kutokana na uhitaji wa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo nchini humu wakaona ni vyema waratibu kambi ya upimaji na matibabu ya moyo na kuwatuma wataalamu wa JKCI kwenda kutoa huduma kwa wananchi wa Malawi.
“Kwa namna ya kipekee ninamshukuru aliyekuwa Balozi wa Malawi Mhe. Humphrey Polepole ambaye alitufuata na kutuomba tukatoe huduma za matibabu ya kibingwa nchini humo kwani kuna uhitaji mkubwa wa huduma hiyo na aliichagua Taasisi yetu kwa kuwa inatoa huduma bora za matibabu ya moyo hapa nchini na katika nchi za Afrika Mashariki na Kati”.
“Baada ya wataalamu wa Taasisi yetu kwenda kutoa huduma nchini Malawi imeonekana kuna wagonjwa wengi wanaohitaji kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwani huduma hizo hazipatikani nchini humo hivyo basi ni nafasi kwa Tanzania kwenda kutoa huduma nchini Malawi na katika nchi za jirani ambazo hazina huduma za kibingwa za matibabu ya moyo”.
“Wagonjwa hawa baada ya kufanyiwa uchunguzi wamepewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi yetu ambako ni karibu na Malawi ukilinganisha na nchi zingine. Kwa kuja kwao hapa nchini nchi yetu itaongeza mapato pia tutakuwa tumeutangaza utalii wa matibabu ambao ni maelekezo na maono ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, alisema Dkt. Kisenge.