Baadhi ya wanafunzi wa Shule za Sekondari wakiwa kwenye maandamano ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yaliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Mvuha, mkoani Morogoro. |
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola Wayoga akihutubia wananchi kwenye Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yanayofanyika mkoani Morogoro hivi karibuni. |
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MTANDAO wa Elimu Tanzania (TEN/MET) umetoa maoni yao juu ya rasimu za sera na mitaala ya elimu iliyotolewa Mei 2023 na Serikali ikiwa ni hatua ya kufanya maboresho zaidi katika sekta ya elimu. Kwa mujibu wa taarifa ya TENMET iliyotolewa Jijini Dodoma, imeshauri Sera itamke wazi nini kifanyike inapotokea majanga katika elimu kwa ngazi zote za elimu na kwa kuwashirikisha pamoja na kuainisha majukumu.
Taarifa hiyo imeipongeza Serikali kwa kukusudia kuleta mapinduzi ya kijamii na kiuchumi ili kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, na kuitaka iangalie namna ya kuvutia na kuajiri waaalimu wenye sifa zinazofaa katika ualimu kwa kuzingatia mwenendo wa tabia nzuri, ufaulu, na uwezo wa fikra tunduizi wa waalimu.
“Jukumu la utolewaji na usimamizi wa elimu lifanywe na wizara ya elimu na TAMISEMI isimamie majukumu mengine. Tuwe na wizara moja mama inayoshughulikia elimu nchini, Serikali ianzishe taasisi inayojitegemea itakayoangalia uthibiti ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu ili kuiongezea nguvu, kuipa rasilimali za kutosha wa kusimamia ubora wa sekta ya elimu nchini,” ilieleza taarifa hiyo.
Aidha wadau hao wa elimu wameshauri shule za binafsi na watoto wanaosoma katika shule hizo wasibaguliwe na kutozwa fedha na malipo mbalimbali ikiwemo ya mitihani na mambo mengine na wasinyimwe pia mikopo ya elimu ya juu huku wakitaka vigezo vya mkopo viwe sawa kwa wote wanaostahili.
Imeshauri elimu sasa kulenga falsafa ya kujitegemea na iendane na uchumi wa nchi ili muhitimu anaposoma na kuhitimu ajue aina ya falsafa inayoendesha uchumi, ama ujamaa au ubebari au mchanganyiko na itamke wazi kwenye sera ili iakisi falsafa inayoendesha uchumi wa nchi.
“…Sera hii ili itekelezeke kwa kipindi kijacho uwekezaji katika elimu uongezwe, hasa katika mafunzo kwa waalimu, idadi ya waalimu wenye sifa iongezwe, ruzuku itolewayo kwa matumizi ya vifaa vya shule za msingi na sekondari iongezwe, namna ya kuwaandaa waalimu watakayoitekeleza sera hii iandane na mahitaji ya sera na watanzania kwa ujumla.
“Elimu ya awali iwe lazima na sera itamke wazi na sehemu ya muda wa elimu ya awali ya mwaka mmoja iwe ni jumla ya muda wa lazima kwa elimu ya msingi nakufanya elimu ya msingi kuwa miaka 11. Elimu ya awali isipopewa umuhimu huu tutadhoofisha uwekezaji katika upatikanaji wa elimu ya awali na kudhoofisha msingi imara wa kujifunza na kusoma hata katika madarasa ya mbele,” imefafanua taarifa hiyo.
Wadau hao wa elimu nchini pia, wameshauri Serikali ihakikishe suala la urejeshwaji wanafunzi waliokatiza masomo katika elimu ya msingi na sekondari kwa sababu mbalimbali ulioanza kutekelezwa 24/11/2021 lina ainiswa wazi katika sera hiyo toleo la 2023 na kuwa sehemu ya tamko.
Pamoja na mambo mengine, wameiomba Serikiali kuhakikisha Bodi ya kitaaluma ya waalimu inaanza utekelezaji wake rasmi sanjari na kufanya mapitio ya haraka kuhusu mpango wa elimu wa miaka mitano 2022/2026, Sheria ya elimu ya mwaka 1978 inaendana na mahitaji ya kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa sera kulingana na ongezeko la watu nchini.