Makatibu wa afya Tanzania wakiwa kwenye mkutano Mkuu wa mwaka unaofanyika kitaifa Jijini Mwanza katika Hoteli ya Gold Crest.
…..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Makatibu wa afya Nchini wametakiwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya pindi wanapofika kwenye vituo mbalimbali vinavyotoa huduma hiyo.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Mei 17, 2023 na Katibu Mkuu wa Wizara ya afya Dkt. Seif Shekalaghe, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa chama cha Makatibu wa afya Tanzania ambao Kitaifa unafanyika Mkoani Mwanza katika ukumbi wa Gold Crest.
Amesema Wizara ya afya imepewa jukumu la kuhakikisha huduma za afya zinafika kwa wananchi tena kwa ubora, ni mkataba wa kijamii uliowekwa baina ya wananchi na Serikali kupitia uchaguzi Mkuu uliofanyika.
Aidha, Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaahidi wanataaluma hao kushughulikia masuala ya uanzishwaji wa baraza la kitaaluma na katika kuboresha Muundo wa kada hiyo ameahidi kuzungumza kwa pamoja na Katibu Mkuu TAMISEMl ili kulipatia ufumbuzi mara moja.
Katika kuboresha huduma, Katibu Mkuu amewaagiza kubaini vikwazo vya watumishi kwenye utoaji wa huduma na kutoa Mapendekezo ya namna ya kuboresha na kwamba katika utendaji wao wajenge upendo baina ya watumishi na kuthamini mchango wa kila mmoja.
Ameongeza kuwa katika utoaji wa huduma za afya kila mmoja anapaswa kuwa na lugha nzuri ya ufariji kwa mgonjwa kabla ya kumhudumia hivyo wanataaluma hao wanapaswa kwenda kusimamia duala hilo kila wakati ili kujenga jamii bora.
Naye, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana, ametoa rai kwa Makatibu wa afya kusimamia maadili ya utumishi wa umma kwa kuwasimamia watoa huduma ili kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma bora za afya na kuitendea haki Miundombinu iliyoboreshwa na Serikali.
Awali akizungumza kwenye kikao hicho Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu wa afya Bi. Juliana Mawala, amebainisha changamoto za kutokua na baraza inapelekea kukwamisha usimamizi wa masuala ya kinidhamu kwa watumishi wa afya na Muundo Mpya kutomtambua katibu wa afya kama Msimamizi Mkuu wa masuala ya wafanyakazi wa kada ya afya kukwamisha kazi zao.