Mbunge wa Jimbo la Ilemela jijini Mwanza Mhe Dkt Angeline Mabula amekabidhi mifuko ishirini ya Saruji kwaajili ya ujenzi wa barabara ya mtaa wa Kilimani ‘B’ kata ya Kirumba ili kuondoka adha ya usafiri Kwa wananchi wa mtaa huo.
Akizungumza wakati wa zoezi la makabidhiano ya Saruji hiyo, Katibu wa Mbunge Kanda ya Kirumba Bi Fatma Karoli amesema kuwa Jimbo la Ilemela limekuwa na desturi ya kufanya kazi kwa utaratibu wa utatu Kwa maana ya wananchi kuanzisha mradi, Mbunge kuunga mkono kwa kuuendeleza mradi huo na kisha manispaa au Serikali kuu kumalizia Kwa kuukamilisha
‘.. Mbunge wetu anatambua adha tunayoipata Kwa ukosefu wa barabara za uhakika, Mlivyoanza akaona awaunge mkono na huu ni utaratibu wake wa kawaida kabisa amefanya hivi kwenye miradi mingi tu ndani ya Jimbo letu ..’ Alisema.
Aidha Bi Karoli amewaasa wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan katika kuwaletea maendeleo pamoja na kumuombea Mbunge wao ili aendelee kuwatumikia
Nae mratibu kutoka ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela Ndugu Mpunzi Mbegeje amesema kuwa Mbunge Dkt Angeline Mabula ataendelea kutatua kero zinazowakabili wananchi wake katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, elimu na miundombinu hivyo kuwaasa viongozi wa kata na mitaa kutoa ushirikiano
Mhe Wessa Juma ni diwani wa kata ya Kirumba ambae amemshukuru Mbunge huyo Kwa msaada wa mifuko ya Saruji itakayosaidia ujenzi wa barabara ya mtaa wa Kilimani ‘B’ kwani imekuwa ikiwatesa wananchi wa kata yake kwa muda mrefu kitendo kilichochangia kukwamisha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi hao kwa kushindwa kufika sokoni na mwaloni Kwa urahisi Ili kufanya shughuli za uzalishaji mali
Nae Mwenyekiti wa mtaa wa Mlimani ‘B’ Bwana Ahmad Manugulilo mbali na kumshukuru Mbunge huyo amewataka wadau wengine wa maendeleo kujitokeza na kuchangia gharama nyengine zitakazofanikisha ujenzi wa barabara hiyo ya mtaa badala ya kutegemea kila kitu kutoka Serikalini
Umrat Ibrahim Kapera ni mwananchi wa mtaa wa Mlimani ‘B’ yeye amewataka viongozi wengine kuiga mfano wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula Kwa namna anavyoshirikiana na wananchi wake katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kutatua kero za wananchi hasa adha iliyokuwa ikiwakabili wanawake wajawazito pindi wanapotaka kujifungua kabla ya kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo