Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo
Muonekano wa dawa aina ya P-500® (Paracetamol) inayotengenezwa na kiwanda cha Apex Laboratories Private Limited-Tamil Nadu-India
………………………….
NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetolea ufafanuzi kuhusu uvumi wa dawa aina ya P-500® (Paracetamol) inayotengenezwa na kiwanda cha Apex Laboratories Private Limited-Tamil Nadu-India kuwa, kiwanda cha dawa hiyo hakitambuliki hapa nchini huku dawa yake hakuna uthibitisho wa kuwepo kwenye soko la Tanzania.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TMDA , Adam Fimbo taarifa yake kwa Umma amebainisha kuwa, Uwepo wa taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu dawa hiyo ya P-500® (Paracetamol) inayoonesha kutengenezwa na kiwanda hicho, kuwa ina virusi aina ya ‘Machupo’ vinavyosababisha ugonjwa wa “Bolivian Hemorrhagic Fever (BHF).
“Taarifa hii imekuwa ikijirudia mara kwa mara na Mamlaka imekuwa ikitolea ufafanuzi kuhusu madai hayo.
TMDA inapenda kuufahamisha Umma kwamba hakuna virusi vijulikanavyo kwa jina la Machupo na pia virusi vya aina yeyote ile haviwezi kuishi kwenye kidonge.” Amesema Fimbo.
Aidha, dawa ya Paracetamol ambayo inatumika kwa ajili ya kutibu maumivu na homa, imesajiliwa hapa nchini kwa majina mbalimbali ya kibiashara baada ya Mamlaka kuthibitisha kuwa ni salama kwa matumizi.
“TMDA inawahakikishia wananchi kupitia mifumo iliyopo itaendelea kufuatilia kwenye soko na mipakani ili kuhakikisha kuwa pamoja na bidhaa nyingine, dawa hiyo ambayo haijasajiliwa haiingii nchini.
Wito unatolewa kwa wananchi kuwa endapo watabaini au kuhisi kwamba dawa walizotumia zimesababisha madhara ya kiafya wasisite kutoa taarifa TMDA kupitia mifumo ya utoaji taarifa za madhara ya dawa kwa njia ya kielektroniki ?Adverse Reaction Reporting tool ) au kujaza fomu maalum na kuziwasilisha katika ofisi za Kanda zilizopo Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Tabora na Geita au kupitia ofisi za Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya.” Imeeleza taarifa.
Hata hivyo, TMDA imewaomba wananchi kutoendelea kusambaza taarifa za uvumi ambazo hazijathibitishwa na kupatiwa ufafanuzi kutoka katika Mamlaka husika kwa kuwa huzua taharuki katika jamii.
TMDA ni Wakala wa Serikali chini ya Wizara ya Afya, yenye jukumu la kudhibiti usalama, ubora na ufanisi wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa za tumbaku.
Ambapo kwa lengo la kujiridhisha kuwa dawa zilizopo nchini zinakidhi usalama, ubora na ufanisi,imeweka mifumo mbalimbali ya udhibiti ikiwa ni pamoja na mifumo ya tathmini na usajili, ukaguzi, uchunguzi wa kimaabara na ufuatiliaji wa usalama na ubora wa dawa kwenye soko.