Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera .
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera amewatoa hofu wakazi wa Kijiji cha Kimotorok Kata ya Loiborsiret juu ya kunyang’anywa kitongoji, hivyo wasubiri maamuzi ya Serikali.
Wakazi wa kijiji cha Kimotorok wameshikwa na sintofahamu na taharuki kubwa baada ya kusikia kitongoji chao cha Arkasupai kimekuwa sehemu ya hifadhi ya Mkungunero.
Inadaiwa kuwa ramani mpya inaonyesha kitongoji chao cha Arkasupai kipo wilaya ya Kondoa, nje ya mpaka wa barabara kuu inayotenganisha mikoa ya Manyara na Dodoma.
Dk Serera akizungumza juu ya hilo, amewataka wakazi hao watulie na kusubiria hatua zaidi kwani mkuu wa mkoa huo Charles Makongoro Nyerere, amefikisha kilio chao sehemu husika.
Amesema mkuu wa mkoa huo baada ya kufika kwenye eneo hilo, amesikiliza kilio cha wakazi hao na kufikisha hoja zao sehemu husika hivyo wasubirie zifanyiwe kazi.
“Niwape pole kwa taharuki mliyopata, tuendelee kuwa watulivu huku tukisubiri mrejesho kutoka kwa viongozi, natumaini hoja mlizozitoa zitasikilizwa,” amesema Dk Serera.
Mkazi wa wilaya hiyo Lowasa Lormuje amewaasa viongozi wengine hasa wa kuchaguliwa waige mfano wa mkuu huyo wa wilaya ambaye yupo karibu na jamii inayomzunguka kwa kila jambo.
“Simanjiro ingepata viongozi watano kama Dk Serera, tutafika mbali kwani ni kiongozi wa kuigwa anayefuatilia jambo kwa ukaribu, hili suala la Kimotorok linapaswa kuchunguzwa kiundani kwani kuna watu wanataka kupora ardhi,” amesema.
Mkazi wa kijiji hicho Karakai Barisha amesema wanamuomba Mungu wakiwa na mshikamano kwani wanaumia mioyoni mwao kuona hali kama hiyo inatokea kwenye eneo lao.
“Jamii inapokuwa na hofu na taharuki ya jambo lolote lile viongozi wanapaswala kueleza hatua iliyofikiwa kuliko kukaa kimya na kuzidisha maumivu mioyoni mwetu,” amesema.