Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lusius Mwenda, akifungua kikao kazi cha Wasimamizi wa Mali za Serikali kutoka Mikoa yote Tanzania Bara (hawamo pichani) kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Bw. Chotto Sendo, akizungumza jambo wakati wa kikaokazi cha Wasimamizi wa Mali za Serikali kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Sera za Manunuzi ya Umma, Dkt. Frederick Mwakibinga, akichangia mada katika mafunzo ya kikao kazi cha Wasimamizi wa Mali za Serikali kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, jijini Dodoma.
Baadhi wa Wasimamizi wa Mali za Serikali kutoka Mikoa ya Tanzania Bara wakisikiliza kwa makini majadiliano katika kikaokazi cha wasimamizi hao kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, jijini Dodoma.
Meza Kuu ikiongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lusius Mwenda (wa tatu kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Chotto Sendo (wa tatu kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa kikaokazi cha Wasimamizi wa Mali za Serikali, kilichofanyika jijini Dodoma
Baadhi ya maofisa katika Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali Wizara ya Fedha na Mipango wakisikiliza kwa makini mafunzo katika kikaokazi cha Wasimamizi wa Mali za Serikali kilichofanyika jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)
…………………….
Na. Eva Valerian na Peter Haule, WFM, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Omolo, ameziagiza Ofisi za Mikoa za Usimamizi wa Mali za Serikali kutoa mafunzo kwa taasisi za umma kuhusu Mfumo wa Usimamizi wa Mali za Serikali (GAMIS) katika maeneo yao ili kuziwezesha kuingiza na kuhuisha taarifa za mali kwenye mfumo kwa wakati.
Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Bw. Lusius Mwenda, wakati wa kikao kazi cha Wasimamizi wa Rasilimali watu kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.
Alisema kuwa Serikali inatenga fedha kila mwaka kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miradi ya maendeleo ambayo utekelezaji wake unaifanya Serikali kuongezeza mali ambazo zinahitaji udhibiti na utunzaji wa mali hizo kwa ajili ya faida ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.
“Mafunzo ya Mfumo wa GAMIS yawezeshe kuingiza na kuhuisha taarifa za mali kwenye mfumo huo kwa wakati na pia kusimamia Mfumo wa GAMIS, uondoshwaji wa mali za umma na kuhakiki taarifa za mali kabla ya kufunga hesabu kama ilivyoelekezwa katika mwongozo wa usimamizi wa mali wa mwaka 2019”, alisema Bw. Mwenda.
Alisema kuwa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali itoe mafunzo wezeshi kwa maafisa usimamizi wa mali za Serikali hususani maafisa wapya kwa lengo la kuwajengea uwezo kwenye matumizi ya moduli zilizopo kwenye Mfumo wa GAMIS
Pia ameitaka Idara hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka na Taasisi nyingine ihakikishe Mfumo wa GAMIS unatumiwa ipasavyo na taasisi zote za Serikali ili kufikia lengo la kuanzishwa kwa Mfumo huo.
Vilevile aliongeza kuwa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2021/2022 imebaini masuala mengi ya usimamizi wa mali ikiwemo magari ya taasisi kuegeshwa kwa muda mrefu bila matengenezo kisha kufutwa au kuondoshwa.
Alisema hoja hizo zilizotolewa na CAG zinapaswa kufanyiwa kazi kwa kuwa Sera, kanuni, miongozo na taratibu zinazosimamia matumizi ya mali za umma ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha mali hizo zinasimamiwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuakisi thamani halisi ya fedha.
Pia alisema kuwa katika jitihada za kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na kuendana na uchumi wa kidigitali, Serikali iliamua kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mali za Serikali (GAMIS) kwa lengo la kuimarisha Mfumo wa usimamizi wa mali za umma pamoja na kuondoa changamoto zilizopo.
Alieleza kuwa matumizi sahihi ya mfumo wa GAMIS hususani moduli mama ya usajili wa mali na moduli nyingine zilizopo katika mfumo huo yataiwezesha Serikali kutambua kiasi, Idadi, hali na mali zilizopo na kuziwezesha taasisi kufunga hesabu za Fedha kwa kutumia taarifa zilizopo katika Mfumo wa GAMIS kama ilivyoelekezwa kupitia waraka wa Hazina Na. 2 wa mwaka 2021/22.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Bw. Chotto Sendo, alisema kuwa Wasimamizi wa Mali za Serikali wanatakiwa kuhakikisha wanatimiza matarajio ya nchi na wananchi katika kuhakikisha majukumu yao yanatekelezwa kwa weledi ili kuleta tija kwa nchi.
Alisema kikao kazi hicho kitasaidia kuongeza uelewa hivyo kufanya kazi kwa bidii na ufanisi katika mazingira yeyote kutokana na mazingira ya majukumu yao.
Alisema kuwa ili kuleta tija miongoni mwa eneo muhimu ni rasilimali watu ambao ni wasimamizi wa mali hizo lakini pia maadili na mifumo ya kiutendaji ambayo ni lazima ifanye kazi vizuri ili kuleta tija.
Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali hufanya kikao kazi kila mwaka kwa kuwakutanisha Wasimamizi wa Mali za Serikali katika mikoa yote Tanzania Bara, ili kufanya tathmini ya kiutendaji na kuangalia namna bora ya kutatua changamoto zilizopo na zitakazojitokeza.
Mwisho.