Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Deogratius Ndejembi akifungua semina ya waandishi wa habari kuhusu shughuli za Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART inayofanyika kwa siku tano kwenye hoteli ya Dodoma City jijini Dodoma.
………………………………………
Na Angela Msimbira DODOMA
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe.Deogratius Ndejembi ametoa rai kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuanza usanifu wa huduma hiyo kwa ajili ya majiji mengine makubwa likiwepo jiji la Dodoma
Ndejembi ameyasema hayo leo Mei 15, 2023 jijini Dodoma wakati wa kufungua mafunzo elekezi kwa waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa mradi wa DART.
Amesema kutokana na majukumu ya wakala huyo ni vyema kuanza mchakato wa kufanya usanifu wa huduma hiyo katika majiji makubwa likiwemo jiji la Dodoma.
“Rai yangu kwa DART ianze kuangalia maenoe mengine kama jiji la Dodoma, mfano kwa sasa TANROADS inaanza ujenzi wa njia nne kutoka Mji wa Serikali hadi katikati ya jiji, hivyo DART mzungumze na TARURA na TANROADS ili kwenye mipango yao waweze kuweka eneo la akiba katikati ya barabara”amesema Ndejembi
Ameendelea kufafanua kua hatua ya kusanifu ikianza mapema itaondoa adha ya kuvunja vunja na kulipa fidia pindi upanuzi wa huduma hii utakapofika kwenye majiji makubwa .
Aidha, Ndejembi amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika Jiji la Dar es Salaam ili kuhakikisha wananchi wanafika katika shughuli zao kwa haraka.
Akielezea utekulezaji wa Mradi wa DART kwa Jiji la Dar-es-salaam Mhe. Ndejembi amesema katika awamu ya kwanza ya mradi Serikali imetumia dola za Marekani milioni 235 wakati awamu ya pili Serikali imetenga dola za Marekani milioni 141 na utekelezaji wake umefikia asilimia 96.
Ndejembi amesema katika awamu ya tatu ya kutoka mjini hadi Gongo la Mboto, Serikali imetenga dola za Marekani milioni 148 na mkandarasi yuko eneo la kazi kuendelea na utekelezaji wa mradi.
Awali, Mkurugenzi wa Utawala, Rasilimali Watu wa DART, Dk Eliphas Mollel alisema Wakala imesaidia sana kuondoa msongamano wa abiria na kuwa kumekuwa na ongezeko la kusafirisha abiria kutoka abiria 50,000 hadi kufikia abiria 200,000 kwa kila siku.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Deogratius Ndejembi akisisitiza jambo wakati akifungua semina ya waandishi wa habari kuhusu shughuli za Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART inayofanyika kwa siku tano kwenye hoteli ya Dodoma City jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Deogratius Ndejembi akipata maelezo kutoka kwa Mohammed Kuganda Meneja Mipango na Usafirishaji DART kabla ya kufungua semina ya waandishi wa habari kuhusu shughuli za Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART inayofanyika kwa siku tano kwenye hoteli ya Dodoma City jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa (TAMISEMI) Dkt. Willson Mahera akimkaribisha Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Deogratius Ndejembi ilikufungua semina ya waandishi wa habari kuhusu shughulia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART inayofanyika kwenye hoteli ya Dodoma City.
Dkt. Eliphas Mollel Mkurugenzi Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala na Kaimu Mtendaji Mkuu DART akitoa hotuba ya utangulii kabla ya kufunguliwa kwa semina hiyo.
PIcha Zikionesha waandishi wa habari mbalimbali wa habari wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi wakati akifungua semina hiyo.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.