Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akizungumza na wananchi wa Itigi (Hawapo Pichani), mara baada ya utiaji saini mkataba wa mradi wa Ujenzi wa Barabara za Maingilio katika Daraja la Sibiti, Noranga-Doroto na Itigi-Mkiwa, Mkoani Singida.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila, akitoa taarifa ya mradi kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa (Hayupo pichani) katika hafla ya utiaji saini mkataba wa mradi wa Ujenzi wa Barabara za Maingilio katika Daraja la Sibiti, Noranga-Doroto na Itigi-Mkiwa, Mkoani Singida.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila pamoja na Mwakilishi kutoka kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd. (CHICO) wakionesha mikataba ya mradi wa Ujenzi wa Barabara za Maingilio katika Daraja la Sibiti , Noranga-Doroto na Itigi-Mkiwa, Mkoani Singida.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila na Mwakilishi kutoka kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd. (CHICO), wakisaini mikataba wa mradi wa ujenzi wa Barabara za Maingilio katika Daraja la Sibiti, Noranga-Doroto na Itigi-Mkiwa, Mkoani Singida.
Baadhi ya Viongozi na Wananchi, Wakishuhudia utiaji saini mkataba wa mradi wa Ujenzi wa Barabara za Maingilio katika Daraja la Sibiti, Noranga-Doroto na Itigi-Mkiwa, Mkoani Singida.
…
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa, Makame Mbarawa amesema Ujenzi wa Barabara za lami unaoendelea na utakaoanza hivi karibuni unalengo la kuufanya mkoa wa Singida kuwa kiunganishi na kitovu cha biashara kwa Mikoa ya kanda ya kaskazini, kati, ziwa na nyanda za juu kusini.
Akizungumza mjini Itigi katika hafla ya utiaji saini, mikataba ya ujenzi wa barabara za maingilio katika daraja la Sibiti zenye urefu wa KM 24.83 na barabara ya Makongolosi-Rungwa-Itigi-Mkiwa, sehemu ya Noranga hadi Doroto (KM 6) na Itigi hadi Mkiwa (KM25.569) kwa kiwango cha lami.
Profesa Mbarawa amewataka wakazi wa Mkoa wa Singida kujipanga kutumia fursa za miradi hiyo kujikwamua kiuchumi.“Ujenzi wa Sehemu ya Noranga – Doroto na Itigi – Mkiwa ni Muendelezo wa juhudi za Serikali kuifungua barabara yote ya Makongorosi-Rungwa -Itigi hadi Mkiwa kwa kiwango cha lami, na hivyo kuinganisha Mikoa ya Singida na Mbeya kwa urahisi zaidi”amesema Profesa Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa amewataka viongozi wa Mkoa wa Singida, kuwapa ushirikiano wa kutosha Mkandarasi China Henan International Cooperation Group Co. Ltd. (CHICO) na wataalamu wengine wanaojenga barabara hizo ili zikamilike katika ubora uliokusudiwa na mapema Zaidi.
“Viongozi wa Mkoa na wa TANROADS, hakikisheni vijana wa mkoa wa Singida wanapata kipaumbele katika kupata ajira kwenye miradi inayoendelea ili kuwawezesha kunufaika kwa kupata utaalamu na kukua kiuchumi”.
Amesisitiza Profesa Mbarawa.Barabara hizo zitakapokamilika zitaunganisha Kirahisi Mikoa ya Singida, Simiyu, Shinyanga , Arusha, Dodoma na Tabora na kufanya mkoa wa Singida kunufaika na Shughuli za kilimo, utalii na biashara.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila amesema kuwa barabara za Maingilio katika daraja la sibiti zitakapokamilika zitaondoaa adha ya usafiri katika daraja la hilo na hivyo kuvutia wasafirishaji wengi kupita njia hiyo.
Eng. Mativila ameongeza kuwa ujenzi huo utahusisha upanuzi wa makaravati makubwa na madogo na ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua kwenye sehemu zenye mmomonyoko wa udongo.
Naye, Mbunge wa Manyoni Magharibi, Mhe Yahaya Masare akizungumza kwa niaba ya Wabunge wa Mkoa wa Singida, ameishukuru Serikali kwa namna inavyotekeleza Miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara mkoani humo, Barabara ya itigi hadi Mkiwa ni Sehemu ya barabara itokayo Mbeya kupitia Makongorosi-Rungwa-itigi hadi Mkiwa yenye urefu wa Kilomita 413 ambapo sehemu ya Mbeya- Lwanjilo hadi Chunya (KM 72), na Chunya – Mkongorosi (KM 39), tayari imekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.
Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa amesema tayari Serikali imeshapata mkandarasi atakayejenga Barabara ya Handeni-Kibirashi hadi Singida (KM 462) na maandalizi ya kusaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Arusha-Kongwa Junction (KM 438), Mbulu-Hydom (KM 400), na Ifakara-Lupilo-Malinyi hadi Namtumbo (KM.480 ) nyatakamilika Mwezi juni mwaka huu.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI