Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi akipokea maandamano ya wauguzi yaliyoongozwa na kikundi cha Brass band cha Magereza wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi Duniani yaliyofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-wakil Kikwajuni Mjini Unguja, Mei 12,2023.
Muuguzi Saida kheir Hamad akisoma Risala ya wauguzi wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi Duniani yaliyofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-wakil Kikwajuni Mjini Unguja,Mei 12,2023.
Mwenyekiti wa Jumuia za Wauguzi Zanzibar (ZANA) Dkt.Rukia Rajab akitoa nasaha kwa wauguzi wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi Duniani yaliyofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-wakil Kikwajuni Mjini Unguja,Mei 12,2023.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi akihutubia wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi Duniani yaliyofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-wakil Kikwajuni Mjini Unguja ,Mei 12,2023. PICHA NA FAUZIA MUSSA- MAELEZO ZANZIBAR
…..
Rahma Khamis, Maelezo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Mwinyi amewataka Wauguzi kufuata maadili,kuwa na huruma na kutumia weledi katika kuwahudumia wagonjwa ili kuwapa faraja katika matatizo yao.
Ameyasema hayo katika maadhimisho ya siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika huko Ukumbi wa Sheikh Idris Abdul-Wakili Kikwajuni Mjini Unguja.
Amesema ni wazi kuwa kazi ya Uuguzi ni kazi ngumu, lakini inahitaji huruma na upendo ,hivyo ni wajibu wa kila Muuguzi kuhakikisha anajitahidi kutumia ujuzi wake ili kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Dkt Mwinyi ameeleza kuwa katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zaidi Serikali inaendelea kuchukua juhudi kubwa kwa kujenga Hospitali za Mikoa na Wilaya zenye vifaa tiba vya kisasa Unguja na Pemba.
“Nawanasihi Wauguzi wote kuzidisha moyo wa upendo na imani kwa wagonjwa wakati wa utendaji wa kazi zenu kwani nyinyi ndio mnaokaa na kuwahudumia wagonjwa usiku na mchana” .alisisitiza Dkt. Mwinyi.
Dkt. Mwinyi amefafanua kuwa ili kuhakikisha huduma bora zinaendelea kupatikana lazima wauguzi washirikiane na kada nyengine ili kufanikisha kazi zao, na kuwashukuru wale wote wanaofanya kazi kwa moyo wa kujitolea.
Hata hivyo Dokt Mwinyi ametoa wito kwa Wauguzi hao kutumia fursa zilizopo za kujiendeleza kielimu ndani na nje ya nchi ili kwenda sambamba na teknolojia na kuja kuimarisha sekta ya Afya nchini kwao.
“kaulimbiu ya maadhimisho haya imeenda sambamba na kazi za uuguzi kwani inaonesha mchango unaofanywa na wauguzi ,hivyo ni wajibu wenu kuendelea kutekeleza majukumu yenu katika Vituo vyote vya Afya Mjini na Vijijini.”Alifahamisha Dkt.Mwinyi
Akitoa nasaha kwa Wauguzi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar (ZANA) Dkt. Rukia Rajab amewataka kutokata tamaa kutokana na changamaoto zinazowakabili na badala yake kuzigeuza changamoto hizo kuwa ni fursa.
Aidha amewasisitiza kuwa na maadili katika kazi zao kwani ni jukumu lao kufanya kazi kwa bidii ili kuikinga jamii na madhara yanayoepukika ikiwemo vifo visivyo vya lazima.
“unapomtibu mgonjwa mmoja na kumrejeshea afya yake imehuisha jamii mzima na unaposababisha kifo cha mtu mmoja umeuwa jamii nzima”alifahamisha Dkt. Rukia
Hata hivyo Dkt Rukia amefahamisha kuwa Siku hiyo ni adhimu kwa wauguzi wote kukaa na kutafakari juu ya kazi zao kwani endapo atamtibu mgonjwa mmoja anapata fungu duniani na akhera.
Maadhimisho ya siku ya Wauguzi Duniani huadhimishwa kila ifikapo mei 12 duniani kote. ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu “WAUGUZI WETU MUSTAKABALI WETU”