Mkuu wa wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa wiki ya Chanjo ambayo kiwilaya imefanyika mjini Tunduru.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro akimpa matone ya kukinga magonjwa mbalimbali mtoto wa wiki sita Vaileth Shungwe,aliyekaa mama wa mtoto Bi Luiza Ndunguru.
Baadhi ya akina mama waliohudhuria uzinduzi wa wiki ya chanjo katika wilaya ya Tunduru,wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo Wakili Julius Mtatiro(hayupo pichani) jana kabla ya uzinduzi rasmi wa zoezi la chanjo.
………………………….
Na Muhidin Amri,
Tunduru
MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro,ameiagiza Halmashauri ya wilaya hiyo kukamilisha haraka mchakato wa kutunga sheria ndogo itakayobana wanaume wenye tabia ya kuwachelewesha wake zao wajawazito kufika katika vituo vya afya kwa wakati.
Mtatiro ameyasema hayo jana wakati,akizindua wiki ya chanjo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na wasichana wenye umri wa maiaka 14 katika zahanati ya Mapambazuko inayomilikiwa na Kanisa Katoriki Jimbo la Tunduru-Masasi.
Alisema,serikali kupitia wizara ya afya imeweka utararibu wa mama anapohisi mjawazito kuwahi kliniki mapema wakati wote wa ujauzito na hata baada ya kujifungua ili kuangalia maendeleo ya afya zao.
Alisema,chanjo inasaidia kuwakinga wajawazito na hatari ya kupata magonjwa na kwa watoto wanaozaliwa kuwa na kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayozulika ikiwemo surua,kupooza,kifua kikuu na kifaduro.
Alisema,kuna watu wanapotosha ukweli kuhusiana na umuhimu wa chanjo ikiwemo chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 walioko shuleni na majumbani kwa kueleza kuwa,ina madhara jambo ambalo halina ukweli.
“chanjo hii ni muhimu sana kwa ajili ya watoto wetu waliopo shule na wale walioko nyumbani,nawaomba wazazi hasa akina mama msikubali kuwasikiliza wapotoshaji,changamkieni chanjo ili kuwaokoa watoto wenu na hatari ya kupata ugonjwa huo”alisema.
Mtatiro amewataka akina mama,kuhakikisha wanakula chakula chenye virutubisho vyote muhimu ili kujenga familia zenye afya bora,badala ya kula chakula cha aina moja kila siku ambacho kinaweza kusababisha tatizo la udumavu na utapiamlo kwa watoto wao.
Amewahimiza wananchi,kuhakikisha wanazingatia na kufuata ushauri unaotolewa na wataalam wa afya ili kujikinga kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali yanayoweza kuepukika.
Katika hatua nyingine,Mtatiro amewakumbusha wananchi juu ya kutunza na kujiwekea akiba ya chakula wanachozalisha kwa ajili ya matumizi ya familia zao na kuepuka tabia ya kuuza chakula chote kutokana na tamaa ya kupata fedha.
Alisema,serikali haitakuwa tayari kutafuta chakula cha msaada kwa watu waliofanya uzembe wa kuuza chakula walichazalisha na kusahau kuweka akiba kwa matumizi yao.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dkt Wilfred Rwechungura alisema,kampeni hiyo imelenga kuwatafuta na kuwafikia kwa wakati watoto wote wanaostahili kupata chanjo hizo ili watoto na akina mama wa Tunduru wanakuwa salama.
Alisema,chanjo hiyo ni muhimu ili kuhakikisha watoto wanakuwa na afya njema na kuwakinga na magonjwa yanayoweza kuzuilika.
Dkt Rwechungura ametoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla, kutoa ushirikiano kwa wataalam waliopo na watakaofika katika maeneo yao ili waweze kutoa huduma hiyo muhimu.
Awali mratibu wa chanjo wilaya ya Tunduru Rose Jemeni alisema,lengo la wiki ya chanjo ni kuwapatia watoto wote na wasichana wenye umri wa miaka 14 ambao hawakupata au hawajakamilisha chanjo kulingana na ratiba ya chanjo.
Alisema,lengo ni kuwakinga na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wake katika kuokoa maisha na kuboresha uchumi na zoezi la hilo litafanyika kwenye vituo vyote vya kutolea huduma kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 11 jioni.
Alisema,tangu kuanza kwa mpango wa chanjo kwa watoto kumekuwa na mafanikio mbalimbali ikiwemo kupungua kwa magonjwa yanayozulika kwa chanjo na jamii kufahamu umuhimu wake.