Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Ormemei Laizer akizungumza na Wakazi wa Kata ya Loiborsiret.
….
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa CCM Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Laizer amezitaka hifadhi za Taifa kusaidia jamii ya wafugaji wanaopakana nao kuliko kuweka kipaumbele cha kukamata mifugo yao pindi ikiingia hifadhini.
Kiria ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya wiki ya jumuiya ya wazazi wa CCM katika kata ya Loiborsiret.
Amesema hifadhi za Taifa zisaidie miradi ya maendeleo kwa kujenga madarasa ya shule, zahanati au maji kwenye vijiji wanavyopakana nao na siyo kuwa na ajenda moja ya kukamata mifugo inayoingia hifadhini.
“Wafugaji waonaishi pembezoni mwa hifadhi ndiyo walinzi namba moja wa wanyamapori hivyo hifadhi za Taifa, zifanikishe miradi ya maendeleo na siyo kukamata mifugo,” amesema Kiria.
Amesema hivi karibuni askari wa hifadhi ya Taifa ya Tarangire walikamata ng’ombe kadhaa za wafugaji wa kijiji cha Kimotorok zilizoingia hifadhini na kuzipiga faini kubwa.
“Hii ni kero kwa sababu huwa wanataka kupiga mnada au kutoza faini kubwa kwa wafugaji hali inayosababisha unyonge kwa wafugaji hivyo pawepo na mahusiano mema,” amesema Kiria.
Hata hivyo, Naibu Katibu mkuu wa jumuiya ya wazazi Taifa (Zanzibar) Othman Ally Maulid, amesema suala la hifadhi kuchangia maendeleo kwa jamii ni zuri ila wafugaji wasiingize mifugo hifadhini.
“Hifadhi zinapaswa kuchangia huduma kwa jamii inayowazunguka ila ninyi wafugaji ndiyo walinzi namba moja wa hifadhi mjitahidi kutoingiza mifugo hifadhini,” amesema Maulid.