New York, Marekani
Ujumbe wa Tanzania ulioko Marekani kuongeza juhudi za kutangaza utalii umeendelea kukutana na wadau muhimu katika kuendelea kutangaza utalii.
Akiwa jijini New York, kama sehemu ya ujumbe unaoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bw. Damasi Mfugale, amekutana na Afisa Mwandamizi wa Mahusiano na Masoko kutoka shirika kubwa la Marekani la Habari la CNN Discovery+ na Eurosport ambapo walijadili pia namna ya kutangaza mchezo wa kimaitaifa wa Tenisi utakaochezwa Serengeti Disemba, 2023 kutangaza utalii.
Akiwa huko pia Bw. Mfugale amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Taasisi inayoongoza duniani kwa kuwaleta pamoja wamiliki wakubwa wa kampuni za utalii ya United States Tour Operators Association (USTOA), Bw. Luis Maravi, ambao wote wameahidi kushirikiana na Tanzania.
Akiwa jijini Los Angeles California, leo Ijumaa, Katibu Mkuu Dkt. Abbasi, katika mwendelezo huo huo anatarajia kukutana na watendaji wa kampuni mashuhuri inayosimamia wasanii wakubwa na mastaa wa Hollywood ili kuona namna ya kuunganisha utalii na sanaa.