Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete leo ametembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jijini Seoul, Korea Kusini na kuzungumza na wafanyakazi. Akiwa na mwenyeji wake Balozi Togolani Mavura, amewahimiza kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na kuunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dkt. Kikwete, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education) – GPE) yuko Seoul, Korea Kusini kwa ajili ya kukutana na viongozi wa Serikali na Mashirika Mbalimbali ya Korea Kusini kwa ajili ya kujadili mikakati ya kuendelea kuboresha elimu katika nchi zinazoendelea. GPE ambayo ilianzishwa na nchi za G7 miaka 20 iliyopita, imeendelea kupigania elimu kwa ajili ya mtoto wa kike na wa kiume kwa kuomba kuungwa mkono na nchi na taasisi zinazoweza kuchangia katika elimu duniani.