Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo ,Halima Okash ,ametoa onyo kali kwa wabakaji na walawiti na kusisitiza zuio la dhamana kwa watuhumiwa hao hasa ambao wamekuwa wakijitamba wanaporejea uraiani baada ya kupata dhamana.
Aidha ameeleza,atakayekutwa na hatia ya kubaka na kulawiti atapigwa picha jamii imfahamu ,ili akirudi uraiani jamii iwe nae chonjo.
Akizungumza na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Chalinze ,Okash alisema ni Lazima kuchukua hatua kali kwani sheria ni msumeno .
Alieleza, kwasasa hakuna nafasi ya kuwakumbatia wanaobainika kubaka na kulawiti ili kupambana na vitendo hivyo wilayani Bagamoyo.
“Utaratibu huu utakuwa unafanywa kwa wanaofanya vitendo hivyo lakini pia jamii itakuwa inawafuatilia kwa karibu watuhumiwa hao ili wasiendelee kufanya vitendo vya kinyama”.
Vilevile,Mkuu huyo wa Wilaya,aliwaasa Maofisa Ustawi wa Jamii kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwa kukaa ofisini pekee badala yake watoke ,waende kwa wananchi kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili.
“Tutafanya ziara kuanzia ngazi ya kata tutashuka mpaka kwenye vijiji kuzungumza na wananchi na watoto wetu, tusipozungumza nao utandawazi utawafunza kwa njia ambayo haitawafunza bali kuzidi kuwapoteza kutoka kwenye maadili” alisisitiza Okash.
Alieleza, wataendelea kufanya hivyo wakiunga jitihada za Rais Samia Suluhu kutokomeza vitendo hivyo vya ukatili kwenye jamii.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze ,Hassan Mwinyikondo aliwataka watendaji wa kata kufanya kazi kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kusimamia fedha za miradi ya maendeleo na kama kuna vikwazo watoe taarifa kwa Mkurugenzi.
Mwinyikondo alisema zipo baadhi ya Kata zimepelekewa fedha lakini hawajazitumia jambo ambalo linasimamisha maendeleo kwenye maeneo husika.
Alihimiza suadilifu kwa watendaji kusimamia shughuli za maendeleo ili kwenda na kasi ya Serikali ya kuleta mabadiliko kwenye jamii kwa fedha za miradi mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa.