Na Mwandishi Wetu, Dar.
IMELEZWA kuwa, Chanjo zinazotolewa kwa watoto nchini ni muhimu katika kulinda afya ya watoto kuepuka magonjwa na vifo ambavyo vingedhuilika kupitia chanjo hizo.
Kauli hiyo imetolewa mapeema jana Mei 9, 20223 na Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam, Ilala Omary Kumbilamoto katika semina ya siku moja kwa Wanahabari jijini Dar es salaam kuhusu huduma za Chanjo nchini ambapo amesema chanjo inauwezo wa kuzuia magonjwa mbalimbali kwa mtoto hivyo kumkinga dhidi ya ugonjwa, ulemavu na hata kifo.
“Mtoto asipopatiwa chanjo anaweza akakumbwa na magonjwa ya mlipuko kama Polio, surua na rubella na kuweza kumsababishia ulemavu au hata kifo” Amesema Kumbilamoto.
Aidha Kumbilamoto amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wakike walio chini ya miaka 14 wanapatiwa chanjo ya Saratani ya shingo ya mlango wa kizazi.
Kwa upande wake Afisa Mpango wa Chanjo Taifa kutoka Wizara ya Afya, Rotalis Gadau amesema kuanzia mwaka 2000 mpaka 2019 kiwango cha huduma za chanjo kiliongezeka kwa kiasi kikubwa kwa takribani asilimia 95% na mwaka 2020 mpaka mwaka 2021 kiwango kilishuka na kufikia asilimia 81% kutokana na Mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona UVIKO-19.
“Baada ya mlipuko wa Uviko-19 Watu wengi waliogopa kufika kwenye vituo vya Afya ili kupata Chanjo wakihofia watoto wao na wao wenyewe kupata UVIKO-19” Amesema Gadau.
Amebainisha kuwa kutokana na mdororo huo wa mwitikio wanajamii kuwachanja watoto wao mwaka 2022 kuliibuka mlipuko wa ugonjwa wa surua na Watoto Takribani 3,923 walibainika kupata ugonjwa huo.
Gadau amebainisha kuwa Mpango wa Taifa wa Chanjo umekuwa ukihakikisha wanajiunga na Kampeni mbalimbali za Afya ikiwemo, kampeni ya HIV, Malaria na RCH ili kutoa Elimu ya chanjo na chanjo ambapo wamekuwa wakijumuika kutoa elimu pia.
Kwa upande wao baadhi ya Waandishi wa Habari, waliahidi kuendelea kushirikiana na Mpango wa Chanjo Taifa katika kutoa Habari sahihi juu ya jamii kupeleka watoto wao kupata chanjo.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa, hadi sasa jumla ya Chanjo 10 zinatumika nchini ambapo zinazuia magonjwa 14, ikiwemo chanjo ya UVIKO 19 ambayo imekuja hivi karibuni.