Na Englibert Kayombo – WAF, Dodoma.
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameitaka Serikali kuweka kupaumbele zaidi kwenye kutoa Elimu na kufanya Kampeni za huduma ya afya ya akili nchini ili wananchi waweze kutambua tatizo hilo na kupata tiba stahiki.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya afya na masuala ya Ukimwi Mhe. Stanslaus Nyongo kwa niaba ya Wabunge wote walioshiriki kwenye Semina maalum ya utoaji Elimu ya Afya ya Akili, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na Bohari kuu ya dawa (MSD) kwa Wabunge iliyofanyika Bungeni Jijini Dodoma.
“Ni vizuri Wizara ikawa na Kampeni maalum ya kutoa elimu ya afya ya akili ili watu wanapotaka kupata huduma za afya ya akili wajue pa kwenda” amesema Mhe. Stanslaus Nyongo
Amesema kampeni hiyo inaweza kuratibiwa kupitia vituo vya ushauri wa masuala ya kitaalam kwa njia za simu (Call Centres), vitengo au vituo vya tiba kwa ajili ya kutibu changamoto za afya ya akili.
“Matangazo na Elimi zikitolewa itapunguza unyanyapaa ndani ya jamii, hali ya aibu itapungua kwakuwa watu watakuwa na uelewa na itawafanya watu kujitokeza kwenda kupata huduma hiyo katika vituo mbalimbali” amesema Mhe. Nyongo.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa, Wizara itaendelea kusimamia huduma za matibabu ya afya ya akili nchini kwa kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma hizo, huku akiwataka wananchi kutoogopa kujitokeza kupata huduma hizo kwa Wataalamu.
“Usione aibu kulia, kulia tiba ya afya ya akili, kwa changamoto ambazo tunapitia ni dhahiri kuwa wananchi wanapata sonona, wanakosa usingizi hizo zote ni changamoto na dalili za afya ya akili” amefafanua Waziri Ummy.
Amesema changamoto ya unyanyapaa kwa watu wenye matatizo ya afya ya akili ni kubwa na hii inaanza kupitia dhana ya mtu akiugua anapelekwa milembe na kuitwa ‘chizi’ ili hali ameenda kupata tiba kama sehemu nyinginezo.
Awali akizungumza Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyoambukiza kutoka WIzara ya Afya Dkt. Omary Ubuguyu amesema kuwa tatizo la afya ya akili ni kubwa duniani na huathiri 13% ya watu wote.
“Takwimu zinaonyesha kuwa kwa Tanzania tatizo la afya ya akili Watanzania kati asilimia 4.2% – 6% wana matatizo ya afya ya akili huku changamoto hizo zikiwaathiri zaidi watu wenye umri wa miaka 15-29” amesema Dkt. Ubuguyu na kuongezea kuwa takwimu hizo za umri hazimaanishi mtu wenye umri zaidi au chini ya hapo hawezi kupata changamoto za afya ya akili.
Amesema Wizara imendelea kutekeleza mkakati wa kuboresha huduma za afya nchini kupitia uongozi, uratibu na usimamizi wa huduma za afya ya akili, kuboresha mfumo wa ukusanyaji takwimu, upatikanaji wa dawa pamoja na kuongeza wataalam zaidi wa masuala ya afya ya akili.