Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Manyara watafanya upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi wa mkoa wa Manyara. Upimaji huo utaenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani yatakayofanyika tarehe 17/05/2023.
Upimaji huo utafanyika kwa watoto na watu wazima kuanzia tarehe 15/05/2023 hadi tarehe 19/05/2023 saa mbili kamili asubuhi mpaka saa 10 kamili jioni katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Manyara.
Kutakuwa na wataalamu wa lishe ambao watatoa elimu ya lishe bora ambayo itawapa wananchi uelewa na kufuata mtindo bora wa maisha ambao utawasaidia kuepukana na magonjwa ya moyo ambayo ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza na yanaweza kuepukika kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.
Watakaogundulika kuwa na matatizo ya moyo watafanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu hapohapo au kupewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi yetu.
Tunawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kupima afya zenu kujua kama mna matatizo ya moyo ili kuanza matibabu mapema kwa atakayebainika kuwa na matatizo.
Kwa taarifa zaidi wasiliana kwa namba 0768408984 Vailine Osward na 0714956529 Abubakar Mjaka.