….
Mahakama ya hakimu mkazi Njombe imelihukumu Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya kusini kulipa fidia ya shilingi Milioni 70 baada ya gari mali ya kanisa hilo kugonga na kusababisha kifo cha marehemu Kaselida Mlowe wa mjini Njombe.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu wa Mahakama ya Hakimu mkazi Njombe Lihad Chamshama amesema mdaiwa namba mbili ambaye ni kanisa anahukumumiwa kulipa fidia ya milioni 70 kutokana na uzembe uliofanywa na mdaiwa namba moja bwana Rajab Kitwana ambaye alikuwa dereva wa gari hiyo wakati ikitoka mjini Makambako kwenye matengenezo na kusababisha kifo cha Marehemu Kaselida.
Mahakama hiyo pia imetoa jukumu kwa kanisa kulipa ghalama zote za uendeshaji wa kesi iliyoendeshwa kwa zaidi ya miaka miwili mpaka sasa huku ikitoa haki ya kukata rufaa kwa kanisa dhidi ya hukumu hiyo.
Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama kutokana na kesi No 2 ya mwaka 2022 ya madai ya fidia ya Milioni 100 dhidi ya kanisa la KKKT iliyofunguliwa na Siglada Mligo msimamizi ambaye ni msimamizi wa mirathi wa marehemu Kaselida Mlowe baada ya kifo kilichotokana na ajali ambapo marehemu aliacha wategemezi wakiwemo watoto wake watatu.
Kesi ilifunguliwa baada ya msimamizi wa mirathi kushinda kesi No 6,2021 ya makosa ya usalama barabarani kutokana na ajali iliyotokea eneo la Kibena Mlima wa Ichunilo mjini Njombe hapo September 25,2020 baina ya Hiace Namba T 298 DNE na gari NO T 210 – AHU Mercedes Benz Track mali ya kanisa na kupelekea kifo cha Kaselida Mlowe.
Kesi hiyo imeendeshwa na Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe Lihad Chamshama huku upande wa madai ukiwakilishwa na mawakili watatu akiwemo Emmanuel Chengula,Frank Ngafumika na Gervas Semgabo huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na wakili Marco Kisakali.