Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Kongamano la Wachimbaji Madini na Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) kwenye ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza, Mei 9, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya washiriki wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua Kongamano la Wachimbaji Madini na Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) kwenye ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza, Mei 9, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
.………………,……..
*Wizara ya Madini imeagizwa kukagua Tozo na Kodi kandamizi*
*Serikali inaendelea kuboresha mazingira mazuri ya biashara ya madini*
Tito Mselem, Mwanahamisi Msangi na Godwin Masabala, Mwanza
Wachimbaji wadogo wa madini wameshauriwa kulitumia Kongamano la wachimbaji wadogo wa Madini kama fursa ya kujiongezea tija na kujipatia kipato cha mtu mmoja mmoja kupitia mafunzo waliyopata.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kwenye kilele cha Wiki ya Maonesho ya Madini wakati akifungua Kongamano la Wachimbaji Wadogo wa Madini na Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) uliofanyika katika ukumbi wa Rock City Mall Jijini Mwanza.
Aidha, Majaliwa amesema kuwa Sekta ya Madini ni Sekta tegemewa inayotarajiwa kuleta matokeo chanya katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kwa Mtanzania mmoja mmoja, Serikali itaendelea kutekeleza adhima yake ya kusimamia na kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini.
“Serikali yetu inathamini sana uchimbaji mdogo kwa kuwa wachimbaji wadogo wanachangia moja kwa moja katika uchumi wetu hivyo Kongamano hili ni muhimu kwa muktadha wa maendeleo ya Sekta ambapo itawaleta karibu wadau wote wa madini na kupata fursa ya kujadiliana ili kupata majibu ya changamoto mbalimbali.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameipongeza FEMATA kwa maandalizi ya Kongamano hilo ambapo amesema mchango wa Sekta ya Madini tangu mwaka 2015 umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka kutokana na usimamizi thabiti unaotokana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wanayoyatoa kwenye sekta hiyo.
Pamoja na mambo mengine Dkt. Kiruswa amesema lengo la Wizara la kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifa ifikapo 2025 litafikiwa na ikiwezekana litachangia zaidi ambapo Wizara kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linaendelea kuwaunganisha wachimbaji wadogo na Taasisi za fedha.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa amefafanua kuwa mchango wa wachimbaji wadogo wa madini umezidi kuimarika kutoka asilimia mbili mwaka 2015 mpaka kufikia asilimia 40 ya makusanyo ya serikali yanayotokana na Mrabaha na ada ya ukaguzi.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima amesema Mkoa wa Mwanza umedhamiria kuwapa leseni wachimbaji wadogo wa madini ambapo wachimbaji wadogo wanawake wamepewa kipaumbele katika kupatiwa maeneo ya uchimbaji madini.
Pia, Malima amemshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika kilele cha kongamano hilo ambapo amesema Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka mpaka kufikia asilimia 9.7 ambapo Mkoa wa Mwanza ni mmoja ya wachangiaji katika ongezeko hilo na kutoa wito kwa washiriki kutembelea vivutio mbalimbali vilivyomo mkoa wa Mwanza ikiwemo visiwa vya Ukerewe na Saa Nane.
Kwa upande wake Rais wa FEMATA John Bina amesema mchango wa Masoko ya Madini umeongezeka kutoka asilimia 2.2 Mwaka 2019 mpaka kufikia asilimia 28 mwaka 2023.
“Hakika tunaiona nguvu ya Mama, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kuilea Sekta ya Madini kwa sasa sekta yetu ya uchimbaji mdogo inazidi kusonga mbele japo kuna changamoto kadhaa ambazo bado tunazifanyia kazi, hakika alipo Mama, Wachimbaji tupo,” amesema Bina.
Aidha, Bina amesema FEMATA imedhamiria kwenda pamoja na wanawake ambapo mpaka sasa takwimu zinaonesha kwamba zaidi ya wanawake 2000 wamejiunga katika shughuli za madini ikiwemo uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani madini.
Awali, akitoa utambulisho wa Viongozi wa Serikali Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesema Kongamano hilo limehudhuriwa na zaidi ya wadau wa madini 1400 ambao wameshiriki katika kutoa elimu mbalimbali kuhusiana na Sekta ya Madini.