Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Bw. Francis Kiwanga (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa “Uraia Wetu” kwaajili ya kukuza uwezo wa AZAKi na kuongeza hamasa na wigo wa ushiriki wa wananchi katika machakato wa katiba mpya. Hafla hiyo imefanyika leo Mei 9, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Meneja programu wa Tanganyika Law Society (TLS) Mackphason Mshana akizungumza katika hafla hiyo kuelezea ushiriki wao katika mchakato wa katiba mpya kupitia mradi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Bw. Francis Kiwanga (kushoto) akimshuhudia Mkurugenzi wa Tanzania Association of NGOs Adamson Nsimba (kulia) akisaini mkataba wa utekelezaji wa Mradi huo, katika hafla fupi iliyofanyika leo Mei 9, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Bw. Francis Kiwanga (kushoto) katika makabiadhiano ya Mkataba wa utekelezaji wa Mradi huo na Meneja programu wa Tanganyika Law Society (TLS) Mackphason Mshana akizungumza katika hafla hiyo kuelezea ushiriki wao katika mchakato wa katiba mpya kupitia mradi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Bw. Francis Kiwanga (kushoto) akitia saini Mkataba wa utekelezaji wa Mradi huo na Taasisi ya Jukwaa la Katiba Tanzania. (kulia) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Bob Wangwe.
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Bw. Francis Kiwanga (kushoto) katika makabiadhiano ya Mkataba wa utekelezaji wa Mradi huo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jukwaa la Katiba Tanzania Bob Wangwe (kulia).
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Bw. Francis Kiwanga (kushoto) akimkabiddhi Mkurugenzi wa Tanzania Association of NGOs Adamson Nsimba (kulia) mkataba wa utekelezaji wa Mradi wa “Uraia Wetu” mara baada ya kutia saini mkataba huo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Bw. Francis Kiwanga (wa pili kushoto) akikabidhi hundi kwa Taasisi zilizosaini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo Jijini Dar es Salaam.
(PICHA NA: FCS)
DAR ES SALAAM
Foundation For Civil Society (FCS) imezindua mradi ujulikanao “Uraia Wetu” utakaotekelezwa kwa miaka mitatu kwaajili ya kukuza uwezo wa AZAKi na kuongeza hamasa na wigo wa ushiriki wa wananchi katika machakato wa katiba mpya pamoja na michakato ya utawala wa kidemokrasia, ikiwa ni pamoja na mapitio ya katiba na maridhiano ya kitaifa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo leo Mei 9, 2023 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Bw. Francis Kiwanga, amesema mradi wa “Uraia Wetu” utachangia kuboresha na kuwezesha mfumo wa sera na mazingira ya ushirikishwaji wa wananchi ili kukuza utawala wa kidemokrasia nchini Tanzania.
“Wananchi wana jukumu kubwa na ni kiungo muhimu cha demokrasia yetu. Mradi wa ‘Uraia Wetu’ unalenga kukuza uhuru wa kujieleza, kupata habari, uhuru wa kukusanyika, na kubaini fursa na nafasi iliyopo kwa wananchi kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya kiraia.
“Tunafahamu kwamba Serikali imepiga firimbi ya kuashiria mwanzo wa mchakato wa maandalizi ya katiba mpya na hivyo sisi kama Foundation For Civil Society tukishirikiana na wadau wenzetu wa maendeleo tumeamua kuja na mpango kabambe wa miaka mitatu wenye lengo la kumfanya kila mwananchi aweze kushiriki katika mchakato wa katiba mpya.
“Tunafahamu katiba yetu ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ibara ya 8 imeweka mamlaka kwa wananchi hivyo hata katika zoezi hili tunalofanya la utengenezaji wa katiba ni lazima tuwaweke wananchi katikati ya mchakato wote wa kupata kabita mpya” amesema Bw. Kiwanga.
Aidha ameeleza kuwa wakati wa mchakato wa marekebisho ya katiba uliopita walijifunza na kuona kwamba wananchi wana nia ya kushiriki katika uundaji wa katiba, na kwamba wanataka kuongezeka kwa uwazi, uwajibikaji, maadili ya kitaifa na juhudi za kweli za kupambana na rushwa.
“Wananchi wana nia ya dhati ya kushiriki katika uundaji wa katiba, wanataka kuongezeka kwa uwazi, uwajibikaji, maadili kitaifa na juhudi za kweli za kupambana na rushwa. Hata hivyo, wakati nafasi ya kiraia ni ndogo, makundi yaliyotengwa kama vile wanawake, vijana, watoto, na watu wenye ulemavu hukabiliana na changamoto, kwani wanakosa majukwaa ya kueleza mawazo yao,” ameeleza Bw Kiwanga ameongeza.
Ameongeza kuwa FCS inaamini kuwa Asasi za Kiraia ngazi za chini zinapowezeshwa na kupata nafasi mwafaka ya kutekeleza majukumu yake ipasavyo, wananchi watafahamu haki zao na kufaidika nazo. Jukumu la asasi za kiraia katika kuendeleza ajenda za wananchi bado ni kubwa na muhimu sana.
“FCS inalenga kuhakikisha watu wanawezeshwa na kuwajibika, na wanapata haki zao za msingi za kiuchumi na kijamii ili kufanya maisha yao kuwa bora. Mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) pia utaimarisha uwezo wa AZAKi ili kukuza ushirikishwaji mzuri kati yao na serikali na wadau wakuu wa maendeleo. Kwa kuongezeka kwa uwezo, AZAKi zitaweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo, na kushirikiana na serikali kushawishi mabadiliko,” Bw Kiwanga ameongeza.
Kwa upande wake Meneja Mipango wa FCS anayehusika na Utawala na Ujumuishwaji wa Jamii, Bi Edna Chilimo, amesema mradi huo unalenga kukuza ushiriki wa asasi za kiraia kwenye michakato ya sera za wadau mbalimbali na kuimarisha uwezo wa AZAKi ili kukuza uwajibikaji wa umma. Mradi unaendana na malengo ya FCS na Umoja wa Ulaya ya kukuza na kulinda haki za binadamu kupitia mazungumzo, utetezi na kujenga uwezo wa ktaalamu.
“Juhudi hizi zinalenga kukuza uhuru wa vyombo vya habari, upatikanaji wa taarifa bora, amani na utatuzi wa migogoro, ushiriki wa wananchi, hasa kwa wanawake na vijana, upatikanaji wa haki kwa makundi ya watu waliotengwa na mipango ya kupambana na rushwa” amesema Bi. Chilimo.
Umoja wa Ulaya (EU) utafadhaili Mradi wa “Uraia Wetu” kwa miaka mitatu kuanzia 2023 hadi 2025 ambapo FCS kama sehemu ya utekelezaji wa mradi huo, imetoa ruzuku ya Tsh 4,916,402,000 kwa AZAKi kumi na mbili (12) za Tanzania Bara na Zanzibar. AZAKI hizo zitaweza kufanya shughuli zitakazochangia katika utekelezaji wa malengo ya mradi huo.
FCS ni Shirika huru la Kitanzania la Maendeleo lisilo la faida ambalo hutoa ruzuku na huduma za kujenga uwezo kwa AZAKi nchini. Tangu kuanzishwa kwake miaka 20 iliyopita, FCS imechangia pakubwa katika kuimarisha uwezo wa asasi za kiraia nchini Tanzania. FCS imeziwezesha AZAKi kuwa chachu ya maendeleo na wananchi kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha utawala wa kidemokrasia nchini Tanzania.