Wakili Melchisedeck Lutema, ambaye ni mwakilishi wa walalamikaji katika ombi lao lililowasilishwa FCT, dhidi ya uamuzi wa FCC akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika kwenye hoteli ya Courtyard Upanga jijiniDar es Salaam leo.
Bernard Elia Kihiyo Mkurugenzi Chama cha Kutetea Walaji na kusemea walaji Tanzania ankifafanua mambo kadhaa katika mkutano huo.
……………………………………………..
Chalinze (Cement) siyo tapeli na Chama cha Kuwasemea Walaji Tanzania siyo tapeli, ni taasisi ambazo zipo kwa mujibu wa sheria na zilikata rufaa kwa mujibu wa sheria na zikapata hukumu kwa mujibu wa sheria siyo wafanya fujo.
Baada ya sakata la kuunganishwa kwa Kampuni ya saruji ya Tanga na Twiga, wadau wakiwemo Kampuni ya saruji Chalinze wamejitokeza na kutaka sheria ifuatwe katika mchakato huo.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Wakili Melchisedeck Lutema, ambaye ni mwakilishi wa walalamikaji katika ombi lao lililowasilishwa FCT, dhidi ya uamuzi wa FCC wa kuidhinisha muungano huo, amesema pande zinazopinga muunganiko wa kampuni hizo, zimefikia uamuzi huo kisheria na hakuna utapeli kama inavyotaka kujengeka.
Ni miaka miwili sasa tangu Tume ya Ushindani (FCC), iridhie muunganiko huo, uamuzi ambao ulibatilishwa na Mahakama ya Ushindani wa Haki (FCT), katika uamuzi wake wa Septemba 23, mwaka 2022, baada ya Kampuni ya Chalinze Cement Limited na Jumuiya ya Kutetea Watumiaji Tanzania (TCAS) kukata rufaa kupinga uamuzi huo.
“Walikidhi vigezo vya sheria kwamba ukiona kuna muunganiko unataka kufanyika lakini ukaona unaweza kuumiza ushindani au ukaathiri matakwa yako au maslahi yako, unaruhusiwa kukata rufaa,” amesema.
Mwanasheria huyo amesema, FCT kwenye uamuzi wake uliopo ukurasa wa mwisho wa 40, ilisema baraza linakataza muunganiko kati ya Scancerm Internatinal DA ambao ni wamiliki wa Twiga Cement na kampuni ya Tanga Cement lakini hivi karibuni .
Amesema katazo hilo maana yake halijawekewa kipindi maalumu, wala masharti yoyote na kwamba ni katazo ambalo ni la kudumu lisilo na maelekezo mengine.
“Kwa hiyo ukiniuliza, hakuna kipindi maalum cha katazo limesema halina muda muda maalum kwamba litadumu muda gani hapa, imekatazwa wakamalizia hapo.
“…Na kwa kuwa hilo katazo halina muda maalum sio sawa kufanya kitu ambacho kimekatazwa mpaka ukitengue na kwa sababu amri ya Mahakama au chombo chochote cha kutoa maamuzi yawe mabaya , mazuri, yanafaa au hayafai, lazima yatekelezwe, labda yatenguliwe kwa njia ya marejeo, mapitio au rufaa,” amesema.
Lutema amefafanua zaidi kuwa, kwa mujibu wa taratibu za kisheria, mtu akiona maamuzi yaliyotolewa hayaendani na matakwa yake anatakiwa aombe marejeo ya hukumu husika.
Amesema kwa sababu hiyo, maamuzi ya FCC yaliyotolewa Februari 28, mwaka huu, kuruhusu tena muunganiko wa Twiga na Tanga Cement yameenda kinyume na hukumu ya FCT.
“Kwa mantiki hiyo, kitu ambacho Chalinze (Cement) na Chama cha Kuwasemea Walaji wamefanya ni kuomba kukata rufaa kwenye Tume ya Ushindani kupinga maamuzi hayo ya Februari 28, rufaa haijaanza kusikilizwa tunasubiri nyaraka kutoka Tume ya Ushindani,” amasema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Kutetea na Kusemea Walaji Tanzania, Bernard Kihiyo, amesema katika kutafuta ufumbuzi wa sakata hilo, wanashauri watoa maamuzi na wasimamia sera, waliingilie kati sakata hilo kwa kuliweka sawa kwa mujibu wa sheria.
“Hakuna uwazi, sasa kuna nini kinachofichwa nchi yetu wote, tuijenge kwa pamoja… tumekuwepo katika hii nchi kwa miaka mingi kama Chama cha Walaji Tanzania hatujawahi kumvuruga mtu hata kwenye ngazi ya nchi, tunafahamu tuna ajenda ya mteja na mteja ndio mwananchi,” amesema.
Mnamo Oktoba 2021, Scancem International DA (Scancem) – kampuni tanzu ya Heidelberg Cement AG, inayomiliki kampuni ya Tanzania Portland Cement Limited Plc (Twiga Cement) – na AfriSam Mauritius Investment Holdings Limited, mmiliki wa Tanga Cement, walikubali kwamba kampuni ya zamani ipate asilimia 68.33. hisa za Tanga Cement
Hata hivyo zabuni ya utwaaji kiwanda hicho cha Saruji cha Tanga ilianzishwa upya Desemba 2022 na Februari 11, 2023, FCC ilitangaza kwamba ilikuwa ikitafuta maoni ya umma kuhusu iwapo upataji huo unapaswa kuidhinishwa au la.