Kassim Nyaki, NCAA
Wajumbe 26 wa taasisi za Uhifadhi kutoka Kenya na Tanzania walioshiriki kikao cha ulinzi wa wanyamapori (Kenya- Tanzania Cross Border Wildlife Security meeting) kilichofanyika jijini Arusha wametembelea Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kujifunza shughuli mbalimbali za uhifadhi, utalii na ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na malikale.
Wataalam hao wa Taasisi za Uhifadhi na Ulinzi kutoka nchi hizo mbili wamekutana jijini Arusha kuanzia tarehe 3-6 Mei, 2023 kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kushirikiana katika utatuzi wa changamoto za kiuhifadhi.
Katika kikao kazi hicho, mada mbalimbali kuhusu ikolojia ya Serengeti- Ngorongoro Masai mara, ikolojia ya Mkomazi-Tsavo magharibi, Ikolojia ya Kilimanjaro-Amboseli na ikolojia ya Tarangire-Manyara ambazo kwa pamoja zinagusa maeneo ya nchi hizo mbili zimejadiliwa.
Katika majadiliano ya wataalam hao kwa pamoja wamekubaliana kudumisha umoja na ushirikiano katika ulinzi na utatuzi wa changamoto za wanyamapori kwa kuwa Wanyamapori hawana mipaka hivyo changamoto za wanyamapori zinavyojitokeza katika hifadhi za nchi hizo lazima zitatuliwe kwa pamoja.