Na Farida Mangube, Morogoro
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA),katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 umepanga kutumia sh bilioni 784 .84 kati ya hizo Sh bilioni 756.19 ni kwa ajili ya miradi ya umeme vijijini na Sh bilioni 28.65 ni kwa masuala ya uendeshaji .
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy alisema hayo katika mkutano wa kwanza wa mwaka kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wadau wa Maendeleo wakiongozwa na Umoja wa Ulaya wanaofadhili miradi ya Wakala huo nchini uliofanyika mjini Morogoro
Mkutano huo ulifunguliwa na Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa ambapo wadau hao walishirikishwa kujulishwa mpango ya Wakala huo na udhibitisho kwao namna inavyosimamiwa katika utekelezaji ukiwemo wa serikali wa kupeleka umeme katika vitongoji vyote nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa REA alisema, kati ya fedha hizo, sh bilioni 350 zitatokana na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa serikali ya Tanzania.
Mhandisi Saidy alisema licha ya bajeti ya Wakala huo ,katika mwaka ujao wa fedha serikali imetenga sh bilioni 377 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji nchini.
Alisema serikali inao mpango mkubwa wa mradi wa kufikisha miundombinu ya umeme katika vitongoji vyote vinavyokadiriwa kufikia 36,101 nchini.
“ Kwa sasa tupo kwenye maandalizi na usanifu ili kujua gharama hasili , lakini vitongoji kati ya 2,300 hadi 2,500 vitapata umeme awamu ya kwanza ya mradi huu “ alisema Mhandisi Saidy
“ Unaweza kuona bado tunahitaji rasilimali fedha na moja ya vitu vimezungumzwa katika mkutano wetu na wabia wa maendeleo wanaotufadhili kwa zaidi ya miaka 10 ni kwenye eneo hili kama wanaweza kutuzaidia vizuri “ alisema Mhandisi Saidy
Mhandisi Saidy alisema licha ya hayo serikali imeshajipanga kuendelea kutekeleza mradi huo kwa awamu mpaka inahakikisha kitongoji cha mwisho kinafikiwa na huduma ya umeme.
Kwa utelekezaji wa mradi mkubwa wa umeme vijijini unaoendelea wa awamu ya tatu mzunguko wa pili alisema, hadi kufikia Aprili mwaka huu vijiji 10,129 kati ya 12,345 vimefikiwa na miundombinu ya umeme.
“ wastani wa asilimia 81 ya vijiji vyote vimevikiwa na umeme na wakandarasi wapo maeneo ya miradi kuweza kuunganisha huduma ya umeme katika vijiji 2,216 zilivyobaki na mpango wetu hadi Desemba mwaka huu viwevimekamilika na kwa baadhi vitakwenda hadi mwanzoni mwa 2024” alisema Mhandisi Saidy
Mhandisi Saidy aliwashukuru wadau wa maendeleo kwani ka kipindi cha miaka mitatu iliyopita walitoa kiasi cha Sh bilioni 659, na kipindi cha mwaka huu wa fedha zimetolewa Sh bilioni 247.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janeth Mbene alisema wadau wa maendeleo wameonesha kufurahishwa na ambavyo Wakala inavyosimamia fedha zinazotolewa na serikali pamoja na wadau wa maendeleo .
Mbene aliwataka watendaji wa Wakala huo kuongeza bdiii katika ufuatiliaji wa miradi hasa Wakandarasi kwa ukaribu zaidi ili waweze kuharakisha kazi zao na kuzimaliza kwa wakati na kwa viwango bora vinavyopaswa kulingana na mikataba yao ilivyoainishwa.
“ Kutokana na kazi hii nzuri iliyofanywa na Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan ya kugharamia miradi ya umeme vijiji na kwenye vitongioji ni jukumu la wananchi kuvuta umeme kwenye nyumba zao , viwanda vyao , kwenye biashara zao na tusimwangushe Rais kwa uwekezaji huu wa hali ya huu uliofanyika” alisema Mbene
Akizungumza kwa niaba ya Wadau wa Maendeleo wakiongozwa na Umoja wa Ulaya wanaofadhili miradi ya REA , Mwakilishi wa Ubalozi wa Norway ( Norwegian Embassy Minister Counseller), Kjetil Schie aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikisha sekta binafsi katika uchangiaji wa shughuli za maendeleo.
Alisema wadau wa maendeleo wataendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo ya Nishati ya umeme vijijini.